Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Sheria 4:32-40

Kumbukumbu la Sheria 4:32-40 BHN

“Fikirini sana juu ya matukio ya zamani, mambo yaliyotukia kabla nyinyi hamjazaliwa, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu duniani. Ulizeni ulimwenguni kote, toka pembe moja hadi nyingine, kama jambo la ajabu la namna hii limepata kutokea au kusikika! Je, watu walikwisha sikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama nyinyi mlivyosikia, wakabaki hai? Je, kuna Mungu yeyote mwingine aliyejaribu kamwe kwenda kujichukulia taifa lake kutoka taifa jingine, kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyofanya, kwa kutumia majaribio, ishara na maajabu, kwa vita na kwa nguvu yake kuu, akasababisha mambo ya kutisha ambayo nyinyi mlishuhudia kwa macho yenu kule Misri? Nyinyi mlijaliwa kuyaona mambo hayo, ili mpate kutambua kwamba Mwenyezi-Mungu, ndiye peke yake Mungu na wala hakuna mwingine. Aliwafanya muisikie sauti yake kutoka mbinguni ili aweze kuwafunza nidhamu; na hapa duniani akawafanya mwone moto wake mkubwa na kusikia maneno yake kutoka katikati ya moto huo. Kwa kuwa aliwapenda wazee wenu, yeye amewateua nyinyi wazawa wao, akawatoa yeye mwenyewe nchini Misri kwa nguvu yake kuu. Aliyafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi, ili awalete na kuwapeni nchi yao iwe urithi wenu, kama ilivyo hadi leo! Basi, kumbukeni leo na kuweka mioyoni mwenu, kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu juu mbinguni na chini duniani; hakuna mwingine. Kwa hiyo shikeni masharti yake na amri zake ambazo ninawapeni leo ili mfanikiwe, nyinyi pamoja na wazawa wenu, na kuishi siku nyingi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni iwe yenu milele.”