Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu la Torati 4:32-40

Kumbukumbu la Torati 4:32-40 SRUV

Tazama siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na kutoka pembe hii ya mbingu hadi ile, kama kumetukia neno lolote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili? Je! Kuna wakati wowote watu wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, na wakaendelea kuishi? Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa kutoka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, ishara, maajabu, vita, mkono hodari, mkono ulionyoshwa, na vitisho vikuu, kama vile BWANA, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu? Wewe umeoneshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amekufanya usikie sauti yake, ili akufundishe; na juu ya nchi alikuonesha moto wake mkuu; ukasikia maneno yake kutoka katika moto. Na kwa sababu aliwapenda baba zenu, kwa sababu hiyo aliwachagua wazao wao baada yao, akakutoa katika Misri kwa kuwako pamoja nawe, kwa uweza wake mwingi, ili kufukuza mbele yako mataifa, walio wakubwa, wenye nguvu kukupita wewe, ili kukuingiza, na kukupa nchi yao iwe urithi, kama ilivyo leo. Kwa hiyo ujue, leo hivi, ukaweke moyoni mwako, ya kuwa BWANA ndiye Mungu katika mbingu juu, na katika nchi chini; hapana mwingine. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo BWANA, Mungu wako, milele.