Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 4:32-40

Kumbukumbu 4:32-40 NENO

Sasa uliza kuhusu siku za zamani, zamani kabla ya wakati wako, tangu siku ile Mungu alipomuumba mtu juu ya nchi, uliza kutoka mwisho mmoja wa mbingu hadi mwisho mwingine wa mbingu. Je, kumepata kutokea jambo jingine lililo kubwa kama hili, au kuna jambo jingine kama hilo limepata kusikiwa? Je, kuna watu wengine wowote waliosikia sauti ya Mungu ikizungumza kwenye moto, kama mlivyosikia, nao wakaishi? Je, kuna mungu yeyote amepata kujaribu mwenyewe kuchukua taifa moja kutoka taifa lingine, kwa mapigo, kwa ishara za miujiza na maajabu, kwa vita, kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyooshwa au kwa matendo makuu ya kutisha, kama yale ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyofanya kwa ajili yenu huko Misri mbele ya macho yenu? Mlioneshwa mambo haya ili mpate kujua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu; hakuna mwingine ila yeye. Kutoka mbinguni amewasikizisha sauti yake ili kuwaadilisha. Hapa duniani aliwaonesha moto wake mkubwa, nanyi mlisikia maneno yake kutoka kati ya ule moto. Kwa sababu aliwapenda baba zenu na alichagua wazao wao baada yao, aliwatoa katika nchi ya Misri kwa Uwepo wake na kwa uwezo wake mkuu, aliwafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko ninyi na kuwaleta ninyi katika nchi yao na akawapa ninyi kuwa urithi wenu, kama ilivyo leo. Kubalini na mweke moyoni leo kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu mbinguni juu na duniani chini. Hakuna mwingine. Mshike amri na maagizo yake ninayowapa leo, ili mpate kufanikiwa ninyi na watoto wenu baada yenu, na mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, siku zote.