Kumbukumbu la Sheria 23:1-14
Kumbukumbu la Sheria 23:1-14 BHN
“Mwanamume yeyote aliyehasiwa au aliyekatwa uume wake haruhusiwi kujiunga na kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Na mwana haramu yeyote, wala mzawa wake hata kizazi cha kumi, haruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Mwamoni au Mmoabu yeyote, wazawa wao wote hata kizazi cha kumi, hawaruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa sababu walikataa kuwapatia chakula na maji mlipokuwa njiani kutoka Misri, na kwa kuwa walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori kule Mesopotamia, awalaani. Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu; badala yake laana hiyo iligeuka kuwa baraka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwapenda. Kwa hiyo, kamwe msiwasaidie hao wapate amani na fanaka. “Msiwachukie Waedomu; hao ni ndugu zenu. Na msiwachukie Wamisri, kwani mlikaa katika nchi yao kama wageni. Wazawa wao, kuanzia kizazi cha tatu, wataruhusiwa kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu. “Mkienda vitani, mkapiga kambi, kila mmoja ajihadhari na kitu chochote kiovu. Kama miongoni mwenu kuna mtu yeyote ambaye ni najisi kwa sababu ya kutokwa mbegu usiku, huyo atatoka nje ya kambi; hatakaa karibu na kambi. Lakini ikifika jioni ataoga, na jua likitua anaweza kurudi kambini. “Lazima muwe na mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda haja. Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na jembe, na hilo mtatumia kuchimba shimo na kufukia kinyesi chenu. Kambi yenu lazima iwe takatifu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anatembea kambini mwenu ili awaokoe na kuwatia adui zenu mikononi mwenu. Kwa hiyo msimwache aone kitu chochote kisichofaa miongoni mwenu, la sivyo atawaacheni.