Kum 23:1-14
Kum 23:1-14 SUV
Aliyejeruhika konde, au aliyekatika tupu yake, asiingie mtu huyo katika mkutano wa BWANA. Mwana wa haramu asiingie katika mkutano wa BWANA; hata kizazi cha kumi asiingie aliye wake katika mkutano wa BWANA. Mwamoni wala Mmoabi wasiingie katika mkutano wa BWANA; wala hata kizazi cha kumi mtu wao asiingie katika mkutano wa BWANA milele; kwa sababu hapo mlipotoka Misri hawakuwalaki na chakula wala maji njiani; na kwa kuwa walimwajiri juu yako Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia, aje akuapize. Lakini BWANA, Mungu wako, hakukubali kumsikiza huyo Balaamu; BWANA, Mungu wako, aliyageuza yale maapizo kuwa ni baraka, kwa vile alivyokupenda BWANA, Mungu wako. Usitafute amani yao wala heri yao siku zako zote, milele. Usimchukie Mwedomi; kwa kuwa ni ndugu yako; usimchukie Mmisri, kwa kuwa ulikuwa mgeni katika nchi yake. Wana wao watakaozaliwa kizazi cha tatu na waingie katika mkutano wa BWANA. Utakapotoka kwenda juu ya adui zako nawe u katika marago, jilinde na kila neno baya. Akiwa kwenu mtu awaye yote asiyekuwa ni tohara kwa ajili ya yaliyomtukia usiku, na atoke nje ya kituo, wala asiingie ndani ya kituo; lakini na iwe ikaribiapo jioni, yeye ataoga maji; na jua likiisha kuchwa ataingia ndani ya kituo. Tena uwe na mahali nje ya kituo, kwa kutokea nje; nawe uwe na jembe dogo katika silaha zako; napo uotamapo nje uchimbe kwa lile jembe, na kugeuka na kukifunika kikutokacho; kwa kuwa BWANA. Mungu wako, yuatembea katika kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako; kwa hiyo na kiwe kitakatifu kituo chako; asije akaona kitu kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha.