Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kumbukumbu 23:1-14

Kumbukumbu 23:1-14 NENO

Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu. Mtu ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi. Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu, hata kizazi cha kumi. Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mkitoka Misri; tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyo Mesopotamia ili awalaani. Hata hivyo, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapenda. Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote. Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake. Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Mwenyezi Mungu. Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi. Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko. Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini. Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia. Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kinyesi chako. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu, akageuka na kuwaacha.