2 Samueli 14:18-33
2 Samueli 14:18-33 BHN
Ndipo mfalme alipomjibu yule mwanamke, “Usinifiche jambo lolote nitakalokuuliza.” Yule mwanamke akasema, “Sema bwana wangu mfalme.” Mfalme akamwuliza, “Je, Yoabu anahusika katika jambo hili?” Yule mwanamke akasema, “Kama uishivyo, bwana wangu mfalme, mtu hawezi kukwepa kulia au kushoto kuhusu jambo ulilosema bwana wangu mfalme. Yoabu yule mtumishi wako ndiye aliyenituma. Ni yeye aliyeniambia maneno yote haya niliyokuambia mimi mtumishi wako. Yoabu alifanya hivyo ili kubadilisha mambo. Lakini, wewe bwana wangu, una hekima kama ya malaika wa Mungu hata unaweza kujua mambo yote yaliyoko duniani.” Kisha, mfalme akamwambia Yoabu, “Sasa sikiliza, natoa kibali changu ili umrudishe nyumbani yule kijana Absalomu.” Yoabu alianguka chini kifudifudi, akasujudu na kumtakia mfalme baraka, akasema, “Leo, mimi mtumishi wako, bwana wangu mfalme, ninajua kuwa nimepata kibali mbele yako, kwa kulikubali ombi langu.” Hivyo, Yoabu aliondoka, akaenda Geshuri kumleta Absalomu mjini Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Absalomu aishi mbali nami; aishi nyumbani kwake. Asije hapa kuniona.” Hivyo, Absalomu akawa anaishi mbali, nyumbani kwake na hakumwona mfalme Daudi. Katika Israeli yote, hakuna yeyote aliyesifiwa kwa uzuri kama Absalomu. Tangu nyayo zake hadi utosini mwake, Absalomu hakuwa na kasoro yoyote. Kila alipokata nywele zake, (na kila mwishoni mwa mwaka alikata nywele zake kwani zilikuwa nzito), alipozipima, zilikuwa na uzito wa kilo mbili kulingana na vipimo vya kifalme. Absalomu alizaa watoto watatu wa kiume pamoja na binti mmoja jina lake Tamari. Tamari alikuwa mwanamke mzuri. Basi, Absalomu aliishi mjini Yerusalemu kwa muda wa miaka miwili mizima bila kumwona mfalme Daudi. Kisha, Absalomu alimtumia ujumbe Yoabu, ili aende kwa mfalme kwa niaba yake, lakini Yoabu akakataa. Absalomu akatuma ujumbe mara ya pili lakini Yoabu akakataa. Basi, Absalomu akawaambia watumishi wake, “Angalieni Yoabu ana shamba la shayiri karibu na langu. Nendeni mkalichome moto.” Kwa hiyo watumishi wa Absalomu wakalichoma moto shamba la Yoabu. Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu akamwuliza, “Kwa nini watumishi wako wamechoma moto shamba langu?” Absalomu akamjibu, “Tazama, nilikupelekea ujumbe, uje huku ili nikutume kwa mfalme, ukamwulize: ‘Kwa nini niliondoka Geshuri? Ingekuwa bora kwangu kubaki huko’. Sasa nisaidie nipate kumwona mfalme. Kama nina hatia basi, na aniue!” Kwa hiyo Yoabu akaenda na kumweleza mfalme maneno hayo yote, naye akamwita Absalomu, naye akaingia kwa mfalme, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme. Na mfalme akambusu Absalomu.