2 Samweli 14:18-33
2 Samweli 14:18-33 NEN
Basi mfalme akamwambia huyo mwanamke, “Usinifiche jibu kuhusu hilo nitakalokuuliza.” Huyo mwanamke akasema, “Mfalme bwana wangu na aseme.” Mfalme akauliza, “Je, mkono wa Yoabu haupo pamoja nawe katika jambo hilo lote?” Huyo mwanamke akajibu, “Hakika kama uishivyo, bwana wangu mfalme, hakuna yeyote anayeweza kugeuka kulia wala kushoto kutokana na chochote anachosema bwana wangu mfalme. Naam, ni mtumishi wako Yoabu ndiye alinifundisha kufanya hivi, naye ndiye aliweka maneno haya yote kinywani mwa mtumishi wako. Mtumishi wako Yoabu amefanya hivi ili kubadili hali iliyopo. Bwana wangu ana hekima kama ile ya malaika wa Mungu, hufahamu kila kitu kinachotokea katika nchi.” Mfalme akamwambia Yoabu, “Vyema sana, nitalifanya jambo hili. Nenda, ukamlete kijana Absalomu.” Yoabu akaanguka kifudifudi mpaka ardhini kumpa mfalme heshima, naye akambariki mfalme. Yoabu akasema, “Leo mtumishi wako anajua kuwa amepata kibali machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa sababu mfalme amemjalia mtumishi wake ombi lake.” Ndipo Yoabu akaenda hadi Geshuri akamrudisha Absalomu Yerusalemu. Lakini mfalme akasema, “Lazima Absalomu aende kwenye nyumba yake mwenyewe; kamwe asiuone uso wangu.” Kwa hiyo Absalomu akaenda kwenye nyumba yake na hakuuona uso wa mfalme. Katika Israeli yote hakuna mtu yeyote aliyesifiwa kwa uzuri wa sura kama Absalomu. Kuanzia utosi wa kichwa chake hadi wayo wa mguu wake hapakuwa na kasoro. Kila mara aliponyoa nywele za kichwa chake, kwa kuwa alikuwa akinyoa mara kwa mara zilipokuwa zinamwia nzito, alizipima uzito wake ulikuwa shekeli mia mbili kwa kipimo cha kifalme. Walizaliwa wana watatu na binti mmoja kwa Absalomu. Jina la binti yake aliitwa Tamari, naye akawa mwanamke mzuri wa sura. Absalomu akaishi miaka miwili huko Yerusalemu pasipo kuuona uso wa mfalme. Basi Absalomu akamwita Yoabu kwa kusudi la kumtuma kwa mfalme, lakini Yoabu akakataa kuja kwa Absalomu. Ndipo akamwita tena mara ya pili, lakini pia akakataa kuja. Ndipo akawaambia watumishi wake, “Tazama, shamba la Yoabu liko jirani na langu, naye ana shayiri humo. Nendeni mkalitie moto.” Kisha watumishi wa Absalomu wakalitia moto shamba hilo. Basi Yoabu akaenda nyumbani kwa Absalomu, akamwambia, “Kwa nini watumishi wako wametia moto shamba langu?” Absalomu akamwambia Yoabu, “Tazama, nilikutumia ujumbe na kusema, ‘Njoo ili niweze kukutuma kwa mfalme kuuliza, “Kwa nini nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa bora zaidi kwangu kama ningebaki huko!” ’ Sasa basi, nataka kuuona uso wa mfalme, na ikiwa nina hatia ya jambo lolote, basi na aniue.” Basi Yoabu akaenda kwa mfalme na kumwambia jambo hili. Kisha mfalme akamwita Absalomu, naye akaingia ndani akasujudu uso wake mpaka ardhini mbele ya mfalme. Naye mfalme akambusu Absalomu.