Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 14:18-33

2 Samweli 14:18-33 SRUV

Ndipo mfalme akajibu, akamwambia yule mwanamke, usinifiche, nakusihi, neno lolote nitakalokuuliza. Na mwanamke akasema, Na anene sasa bwana wangu mfalme. Mfalme akasema, Je! Si mkono wa Yoabu ulio pamoja nawe katika haya yote? Mwanamke akajibu, akasema, Kama iishivyo roho yako, bwana wangu, mfalme, hapana mtu awezaye kugeuka kwa kulia, au kwa kushoto, kukana neno lolote alilolisema bwana wangu mfalme; kwani mtumishi wako Yoabu ndiye aliyeniamuru, na kuyaweka maneno haya yote kinywani mwa mjakazi wako; mtumishi wako Yoabu ameyatenda haya ili kubadili uso wa jambo hili; na bwana wangu anayo akili, kama akili ya malaika wa Mungu, hata ajue mambo yote ya duniani. Basi mfalme akamwambia Yoabu, Angalia sasa, nimekata shauri hili; nenda, ukamrudishe tena yule kijana Absalomu. Naye Yoabu akaanguka kifudifudi hadi chini, akasujudu, akambariki mfalme, Yoabu akasema, Leo mimi mtumwa wako ninajua ya kwamba nimepata neema machoni pako, bwana wangu mfalme, kwa kuwa mfalme amemfanyia mtumishi wake haja yake. Basi Yoabu akaondoka, akaenda Geshuri, akamleta Absalomu Yerusalemu. Naye mfalme akasema, Ageukie nyumbani kwake, asinione uso wangu. Basi Absalomu akarejea nyumbani kwake, asimwone uso mfalme. Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake. Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso. Absalomu akakaa miaka miwili mizima katika Yerusalemu; asimwone uso mfalme. Ndipo Absalomu akatuma Yoabu aitwe, amtume kwa mfalme, lakini yeye akakataa kumjia; akatuma tena mara ya pili, lakini akakataa kuja. Kwa hiyo akawaambia watumishi wake, Tazameni, shamba la Yoabu liko karibu na shamba langu, naye ana shayiri huko; nendeni mkalitie moto. Basi watumishi wa Absalomu wakalitia moto lile shamba. Ndipo akaondoka Yoabu, akamwendea Absalomu nyumbani kwake, akamwambia, Kwa nini watumishi wako wamelitia moto shamba langu? Absalomu akamjibu Yoabu, Angalia, nilituma kwako, nikisema, Njoo kwangu, ili nikutume kwa mfalme kunena, Mbona nimekuja kutoka Geshuri? Ingekuwa heri kwangu kama ningekuwako huko hata sasa; basi sasa na nimtazame uso mfalme; na ukiwapo uovu kwangu, na aniue. Basi Yoabu akamwendea mfalme, akamwambia hayo, naye alipomwita Absalomu, yeye akaja kwa mfalme, akainama kifudifudi hadi chini mbele ya mfalme; naye mfalme akambusu Absalomu.