Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 18:28-37

2 Wafalme 18:28-37 BHN

Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hivi ndivyo anavyosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa mikononi mwa mfalme. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa na mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Msimsikilize Hezekia, maana mfalme wa Ashuru anasema, ‘Muwe na amani nami, na jisalimisheni kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe, matunda ya mtini wake mwenyewe, na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe, mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapeleka mbali katika nchi kama hii yenu, nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mikate na mashamba ya mizabibu; nchi yenye mizeituni na asali, ili mpate kuishi, msije mkafa.’ Msimsikilize Hezekia anapowahadaa akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa.’ Je, kuna yeyote kati ya miungu ya mataifa aliyeokoa nchi yake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru? Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi. Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria mikononi mwangu? Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao mikononi mwangu hata Mwenyezi-Mungu aweze kuukoa mji wa Yerusalemu?” Lakini watu wote walinyamaza kimya, wala hawakumjibu neno, kama walivyoamriwa na mfalme Hezekia, akisema, “Msimjibu.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi, wakamwendea Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruka, wakamweleza maneno ya jemadari mkuu.