Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Fal 18:28-37

2 Fal 18:28-37 SUV

Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake. Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule amiri.