2 Wafalme 18:28-37
2 Wafalme 18:28-37 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa lugha ya Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hivi ndivyo anavyosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa mikononi mwa mfalme. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa na mji huu hautatiwa mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ Msimsikilize Hezekia, maana mfalme wa Ashuru anasema, ‘Muwe na amani nami, na jisalimisheni kwangu. Hapo kila mmoja wenu ataweza kula matunda ya mzabibu wake mwenyewe, matunda ya mtini wake mwenyewe, na kunywa maji ya kisima chake mwenyewe, mpaka baadaye nitakapokuja na kuwapeleka mbali katika nchi kama hii yenu, nchi yenye nafaka na divai, nchi yenye mikate na mashamba ya mizabibu; nchi yenye mizeituni na asali, ili mpate kuishi, msije mkafa.’ Msimsikilize Hezekia anapowahadaa akisema, ‘Mwenyezi-Mungu atatuokoa.’ Je, kuna yeyote kati ya miungu ya mataifa aliyeokoa nchi yake kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru? Je, iko wapi miungu ya Hamathi na Arpadi. Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria mikononi mwangu? Ni nani miongoni mwa miungu ya nchi hizi aliyeokoa nchi zao mikononi mwangu hata Mwenyezi-Mungu aweze kuukoa mji wa Yerusalemu?” Lakini watu wote walinyamaza kimya, wala hawakumjibu neno, kama walivyoamriwa na mfalme Hezekia, akisema, “Msimjibu.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia, Shebna katibu na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi, wakamwendea Hezekia huku mavazi yao yakiwa yameraruka, wakamweleza maneno ya jemadari mkuu.
2 Wafalme 18:28-37 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake. Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule amiri.
2 Wafalme 18:28-37 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu. Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini BWANA kwa kuwaambia, ‘Hakika BWANA atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’ “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe, mpaka nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima, sio mauti! “Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha asemapo, ‘BWANA atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi BWANA aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?” Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.” Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia yale jemadari wa jeshi aliyoyasema.
2 Wafalme 18:28-37 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha yule kamanda akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru. Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake. Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe; hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wowote na mkono wa mfalme wa Ashuru? Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu? Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu? Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno. Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule kamanda.