Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 20:20-30

2 Mambo ya Nyakati 20:20-30 BHN

Kesho yake, wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda mpaka katika jangwa la Tekoa. Walipokuwa wanaondoka, Yehoshafati alisimama, akawaambia, “Nisikilizeni, enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtakuwa imara. Muwe na imani na manabii wake, nanyi mtafaulu.” Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, maana fadhili zake zadumu milele!” Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa. Watu wa Amoni na wa Moabu wakawashambulia wenyeji wa mlima Seiri, na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kuwaangamiza wakazi wa mlima Seiri wakaanza kushambuliana wao kwa wao, wakaangamizana. Jeshi la Yuda lilipofika penye mnara wa ulinzi huko jangwani, waliangalia upande wa maadui, wakaona maiti zimetapakaa kila mahali. Hakuna mtu yeyote aliyenusurika. Yehoshafati na wanajeshi wake wakaenda kuchukua nyara wakakuta ng'ombe wengi, mali, nguo na vitu vingine vya thamani. Iliwachukua muda wa siku tatu kusomba nyara hizo, na hata hivyo, hawakuzimaliza kwani zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Sifa, na kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa yote aliyowafanyia. Ndio maana bonde hilo linaitwa Bonde la Sifa hadi hivi leo. Kisha Yehoshafati akawaongoza wanajeshi wake mpaka Yerusalemu kwa shangwe, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwashinda maadui zao. Walipofika Yerusalemu, walikwenda moja kwa moja hadi nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakipiga vinanda, vinubi na tarumbeta. Falme zote ziliingiwa na hofu ziliposikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowashinda maadui za Israeli. Basi, Yehoshafati akatawala kwa amani, na Mungu akampa amani pande zote.