Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 20:20-30

2 Nyakati 20:20-30 NEN

Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini BWANA Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa. Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia BWANA na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema: “Mshukuruni BWANA kwa kuwa upendo wake wadumu milele.” Walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa. Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao. Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika. Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka kwa maana huko ndiko walikomsifu BWANA. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka mpaka leo. Kisha watu wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kwa kuwa BWANA alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao. Wakaingia Yerusalemu na kwenda hekaluni mwa BWANA wakiwa na vinubi, zeze na tarumbeta. Hofu ya Mungu ikazipata falme zote za nchi waliposikia jinsi BWANA alivyokuwa amepigana dhidi ya adui za Israeli. Ufalme wa Yehoshafati ukawa na amani, kwa kuwa Mungu wake alikuwa amemstarehesha pande zote.