2 Mambo ya Nyakati 20:20-30
2 Mambo ya Nyakati 20:20-30 SRUV
Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao juu ya Waamoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja kushambulia Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwashambulia wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakaanza kuuana wao kwa wao. Hata Yuda walipofika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakakuta miongoni mwao mifugo wengi sana, mali, mavazi na vitu vya thamani, walivyojinyakulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana. Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipomtukuza BWANA; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo. Kisha wakarudi, kila mtu wa Yuda na Yerusalemu, na Yehoshafati mbele yao, ili kuurudia Yerusalemu kwa furaha; kwa kuwa BWANA amewafurahisha juu ya adui zao. Wakafika Yerusalemu wenye vinanda, vinubi na parapanda kwenda nyumbani kwa BWANA. Ikawa hofu ya Mungu juu ya falme zote za nchi, waliposikia ya kuwa BWANA amepigana juu ya adui za Israeli. Basi ukatulia ufalme wake Yehoshafati; kwa sababu Mungu wake alimstarehesha pande zote.