Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wathesalonike 5:14-28

1 Wathesalonike 5:14-28 BHN

Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. Msimpinge Roho Mtakatifu; msidharau unabii. Pimeni kila kitu: Zingatieni kilicho chema, na kuepuka kila aina ya uovu. Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. Ndugu, tuombeeni na sisi pia. Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.