1 The 5:14-28
1 The 5:14-28 SUV
Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote. Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. Ndugu, tuombeeni. Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.