1 Wathesalonike 5:14-28
1 Wathesalonike 5:14-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote. Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote. Furahini daima, salini kila wakati na kuwa na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu. Msimpinge Roho Mtakatifu; msidharau unabii. Pimeni kila kitu: Zingatieni kilicho chema, na kuepuka kila aina ya uovu. Mungu mwenyewe anayetupatia amani awatakase nyinyi kabisa kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu – roho, mioyo na miili yenu – mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye anayewaita nyinyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu. Ndugu, tuombeeni na sisi pia. Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo. Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii. Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
1 Wathesalonike 5:14-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu, tunawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote. Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. Ndugu, tuombeeni. Wasalimieni ndugu wote kwa busu takatifu. Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.
1 Wathesalonike 5:14-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu, twawasihi, waonyeni wale wasiokaa kwa utaratibu; watieni moyo walio dhaifu; watieni nguvu wanyonge; vumilieni na watu wote. Angalieni mtu awaye yote asimlipe mwenziwe mabaya kwa mabaya; bali siku zote lifuateni lililo jema, ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. Ndugu, tuombeeni. Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. Nawaapisha kwa Bwana, ndugu wote wasomewe waraka huu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi.
1 Wathesalonike 5:14-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote. Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote. Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu. Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu; msiyadharau maneno ya unabii. Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema. Jiepusheni na uovu wa kila namna. Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo. Ndugu, tuombeeni. Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu. Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.