Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 10:1-13

1 Wafalme 10:1-13 BHN

Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, kwa sababu ya jina la Mwenyezi-Mungu, alimwendea Solomoni ili kumjaribu kwa maswali magumu. Aliwasili akiwa amefuatana na msafara wa watu pamoja na ngamia waliobeba manukato, zawadi nyingi sana na vito vya thamani. Naye Solomoni akayajibu maswali yote; hapakuwa na swali lolote lililomshinda. Malkia wa Sheba alishangaa sana alipoiona hekima yote ya Solomoni, na nyumba aliyokuwa ameijenga; tena alipoona chakula kilicholetwa mezani mwake, jinsi maofisa walivyoketi mezani, jinsi watumishi walivyohudumu na walivyovalia, pia wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliduwaa na kushangaa mno. Basi, akamwambia mfalme, “Mambo yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni kweli! Lakini sikuweza kuamini habari hizo mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe. Kumbe sikuambiwa hata nusu yake; hekima yako na fanaka zako vimepita habari nilizopewa. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao wanakuhudumia daima na kusikiliza hekima yako! Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa nawe, akakuweka juu ya kiti cha enzi cha Israeli! Kwa sababu Mwenyezi-Mungu alipenda Israeli milele, amekuweka wewe uwe mfalme, ili udumishe haki na uadilifu.” Kisha malkia akampa mfalme zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu, kiasi kikubwa cha manukato na vito vya thamani. Manukato kiasi kikubwa kama hicho alichomtolea mfalme Solomoni hakijapata kamwe kuletwa tena. Tena, msafara wa meli za Hiramu ulioleta dhahabu kutoka Ofiri, ulileta kwa wingi miti ya msandali na vito vya thamani. Naye mfalme aliitumia miti hiyo ya msandali kwa ajili ya nguzo za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na za ikulu na pia kwa kutengenezea vinubi na vinanda vya waimbaji. Kiasi cha miti ya msandali kama hicho hakijaonekana tena mpaka leo. Mfalme Solomoni naye alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na alichotaka; pamoja na vitu vingine ambavyo Solomoni alimpa kutokana na ukarimu wake wa kifalme. Basi malkia akarudi nchini kwake pamoja na watumishi wake.