1 Wafalme 10:1-13
1 Wafalme 10:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, kwa sababu ya jina la Mwenyezi-Mungu, alimwendea Solomoni ili kumjaribu kwa maswali magumu. Aliwasili akiwa amefuatana na msafara wa watu pamoja na ngamia waliobeba manukato, zawadi nyingi sana na vito vya thamani. Naye Solomoni akayajibu maswali yote; hapakuwa na swali lolote lililomshinda. Malkia wa Sheba alishangaa sana alipoiona hekima yote ya Solomoni, na nyumba aliyokuwa ameijenga; tena alipoona chakula kilicholetwa mezani mwake, jinsi maofisa walivyoketi mezani, jinsi watumishi walivyohudumu na walivyovalia, pia wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliduwaa na kushangaa mno. Basi, akamwambia mfalme, “Mambo yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni kweli! Lakini sikuweza kuamini habari hizo mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe. Kumbe sikuambiwa hata nusu yake; hekima yako na fanaka zako vimepita habari nilizopewa. Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao wanakuhudumia daima na kusikiliza hekima yako! Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa nawe, akakuweka juu ya kiti cha enzi cha Israeli! Kwa sababu Mwenyezi-Mungu alipenda Israeli milele, amekuweka wewe uwe mfalme, ili udumishe haki na uadilifu.” Kisha malkia akampa mfalme zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu, kiasi kikubwa cha manukato na vito vya thamani. Manukato kiasi kikubwa kama hicho alichomtolea mfalme Solomoni hakijapata kamwe kuletwa tena. Tena, msafara wa meli za Hiramu ulioleta dhahabu kutoka Ofiri, ulileta kwa wingi miti ya msandali na vito vya thamani. Naye mfalme aliitumia miti hiyo ya msandali kwa ajili ya nguzo za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na za ikulu na pia kwa kutengenezea vinubi na vinanda vya waimbaji. Kiasi cha miti ya msandali kama hicho hakijaonekana tena mpaka leo. Mfalme Solomoni naye alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na alichotaka; pamoja na vitu vingine ambavyo Solomoni alimpa kutokana na ukarimu wake wa kifalme. Basi malkia akarudi nchini kwake pamoja na watumishi wake.
1 Wafalme 10:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno aliloshindwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na maofisa wake walivyokaa, na kuhudumu kwao wahudumu wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na sadaka zake za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa BWANA amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia moja na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani. Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani. Mfalme akafanya kwa miti hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya BWANA, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo. Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
1 Wafalme 10:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la BWANA, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA, roho yake ilizimia. Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa BWANA amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani. Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani. Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya BWANA, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo. Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
1 Wafalme 10:1-13 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la BWANA, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la BWANA, alipatwa na mshangao. Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako! Ahimidiwe BWANA Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake BWANA wa milele ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.” Naye akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni. (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo ya Hekalu la BWANA na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa au kuonekana humo tangu siku ile.) Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.