Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 10:1-13

1 Wafalme 10:1-13 NEN

Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la BWANA, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana: pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani; alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Solomoni akamjibu maswali yake yote, hakukuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika hekalu la BWANA, alipatwa na mshangao. Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako! Ahimidiwe BWANA Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake BWANA wa milele ajili ya Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.” Naye akampa mfalme talanta 120 za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezi na vito vya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa tena vikolezi vingi hivyo kuletwa kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni. (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena kutoka huko zilileta shehena kubwa ya miti ya msandali na vito vya thamani. Mfalme akatumia miti ya msandali kuwa nguzo ya Hekalu la BWANA na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha msandali hakijawahi kuingizwa au kuonekana humo tangu siku ile.) Mfalme Solomoni akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.