Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 10:1-13

1 Wafalme 10:1-13 NENO

Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Sulemani na uhusiano wake na jina la Mwenyezi Mungu, akaja kumjaribu kwa maswali magumu. Alifika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana wenye ngamia waliobeba vikolezo, dhahabu nyingi, na vito vya thamani. Akaenda kwa Sulemani na kuzungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake. Sulemani alimjibu maswali yake yote; hapakuwa na jambo lolote lililokuwa gumu kwa mfalme hata asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa alizotoa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, alipatwa na mshangao mkubwa. Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini mambo haya hadi nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wanaosimama mbele yako daima na kusikia hekima yako! Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka kwenye kiti cha ufalme cha Israeli. Kwa sababu ya upendo wake Mwenyezi Mungu wa milele kwa Israeli, amekufanya mfalme, ili kudumisha haki na uadilifu.” Naye akampa mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu, kiasi kikubwa sana cha vikolezo na vito vya thamani. Kamwe havijawahi kuletwa tena vikolezo vingi kama vile malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Sulemani. (Meli za Hiramu zilileta dhahabu kutoka Ofiri; tena zikaleta shehena kubwa ya miti ya msandali, na vito vya thamani kutoka huko. Mfalme alitumia miti ya msandali kutengenezea nguzo za Hekalu la Mwenyezi Mungu na za jumba la kifalme, na kutengenezea vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Miti mingi ya msandali kiasi hicho haijawahi kuletwa au kuonekana tangu wakati ule.) Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na kukiomba, kando na vile mfalme alivyokuwa amempa kwa ukarimu wake wa kifalme. Kisha malkia akaondoka na kurudi katika nchi yake, yeye na watumishi wake.