Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo ya Mitume 7

7
Stefano mbele ya wakuu.
1Mtambikaji mkuu alipomwuliza: Ndivyo, yalivyo mambo haya? 2akasema: Waume ndugu na baba, sikilizeni! Mungu mwenye utukufu alimtokea baba yetu Aburahamu, alipokaa Mesopotamia, alipokuwa hajahamia Harani,#1 Mose 11:31; 15:7. 3akamwambia:
Toka katika nchi yako kwenye ndugu zako,
uende katika nchi, nitakayokuonyesha!#1 Mose 12:1. 4Ndipo, alipotoka katika nchi ya Wakasidi, akahamia Harani. Tena, baba yake alipokwisha kufa, akamhamisha toka huko, akamweka katika nchi hii, mnayoikaa ninyi sasa.#1 Mose 11:32; 12:5. 5Lakini hakumpa fungu humu, ingawa liwe limelingana na wayo; ila alipokuwa hana mtoto, aliagana naye, ya kuwa atampa, aitwae nchi hii yeye nao wa uzao wake wajao nyuma yake.#1 Mose 13:15. 6Kisha Mungu akavisema: Wao wa uzao wake watakaa ugenini katika nchi ngeni, wale wawafanyishe kazi za watumwa na kuwasumbua vibaya miaka 400.#1 Mose 15:13-14; 2 Mose 12:40. 7Nalo taifa lile, ambalo watalifanyika kazi za watumwa, nitawahukumu mimi, wale wapate kuhama huko, wanitumikie mahali hapa; ndivyo, alivyosema Mungu. 8Kisha akampa agano la tohara; kwa hiyo alipomzaa Isaka akamtahiri siku ya nane; naye Isaka akamzaa Yakobo, naye Yakobo akawazaa babu zetu wakuu kumi na wawili.#1 Mose 7:10. 9Wale babu zetu wakuu wakamwonea Yosefu wivu, wakamwuza kwenda Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye,#1 Mose 37:28; 39:1-2,21. 10akamwokoa katika maumivu yake yote, akamgawia kipaji cha werevu wa kweli, apate kusema mbele ya Farao, mfalme wa Misri; ndiye aliyemweka kuwa mkubwa, aitawale Misri na nyumba yake yote.#1 Mose 41:38-45. 11Njaa ilipokuja kuiingia Misri yote na Kanaani, yakawa maumivu makubwa, baba zetu nao wasione vya kujishibisha. 12Lakini Yakobo aliposikia, ya kuwa Misri ziko ngano, akawatuma baba zetu mara ya kwanza.#1 Mose 42:1-2. 13Katika safari ya pili Yosefu akajitambilisha kwa ndugu zake, nako kwa Farao ukoo wa Yosefu ukajulika.#1 Mose 45:3,16. 14Kisha Yosefu akatuma watu, akamwita baba yake Yakobo na ndugu zake wote, wakawa kama 75.#1 Mose 45:9-11. 15Ndipo, Yakobo alipotelemka kwenda Misri. Huko akafa yeye mwenyewe nao baba zetu,#1 Mose 46:1; 49:33. 16wakapelekwa Sikemu, wakazikwa katika kaburi, alilolinunua Aburahamu na fedha kwa wana wa Hamori kule Sikemu.#1 Mose 23:16-17; 50:13; Yos. 24:32.
Mambo ya Mose.
17Siku zilipokaribia, Mungu alizoziagana na Aburahamu na kujiapisha, watu wa kwetu wakazidi kuwa wengi sana huko Misri,#2 Mose 1:7. 18mpaka alipoondokea mfalme mwingine wa Misri asiyemjua Yosefu. 19Huyo akawaendea wao wa kizazi chetu kwa udanganyi, akawatendea baba zetu maovu akiagiza, vitoto vyao vichanga watupwe, wasikae kuwa wazima.#2 Mose 1:22. 20Siku zile Mose akazaliwa, Mungu akapendezwa naye. Kwa hiyo akalelewa miezi mitatu nyumbani mwa baba yake;#2 Mose 2:2; Ebr. 11:23. 21kisha alipotupwa, binti Farao akamwokota, akamlea, awe mwanawe yeye.#2 Mose 2:10. 22Naye Mose akafundishwa ujuzi wote wa Wamisri, akawa mwenye nguvu kwa maneno na kwa matendo yake.
23Tena miaka yake ilipopata 40, moyo wake ukamtuma kuwakagua ndugu zake, wale wana wa Isiraeli.#2 Mose 2:11. 24Alipoona, mmoja anavyoumizwa bure tu, akamsaidia yule aliyepigwa, akamlipiza yule Mmisri akimwua. 25Akadhani, ndugu zake watajua, ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake yeye; lakini hawakujua. 26Kulipokucha, akawajia tena, akawaona, wakipigana; akawaamua, wapatane, akisema: Waume, ninyi m ndugu, mbona mnakorofishana? 27Lakini yule aliyemkorofisha mwenziwe akamsukuma akisema: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkuu mwamuzi kwetu? 28Je? Wewe unataka kuniua nami, kama ulivyomwua jana yule Mmisri? 29Kwa ajili ya neno hilo Mose akakimbia, akawa mgeni katika nchi ya Midiani. Ndiko, alikozaa wana wawili.#2 Mose 2:15; 18:3-4.
30Ilipokwisha pita tena miaka 40, malaika akamtokea porini mlimani kwa Sinai katika kichaka kilichowaka moto.#2 Mose 3:2; 5 Mose 33:16. 31Mose alipoyaona hayo akastaajabu; lakini alipopakaribia kuyatazama akasikia, Bwana akisema: 32Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Aburahamu na wa Isaka na wa Yakobo. Ndipo, Mose alipotetemeka, hakupata moyo wa kupatazama.#2 Mose 3:6. 33Naye Bwana akamwambia: Vivue viatu miguuni pako! Kwani hapa, unaposimama, ni nchi takatifu. 34Nimeyaona mateso yao walio ukoo wangu walioko Misri; nikasikia, wanavyopiga kite, nikashuka, niwaokoe. Sasa njoo! Nitakutuma, uende Misri. 35Huyo Mose, waliomkataa na kusema: Yuko nani aliyekuweka kuwa mkubwa na mwamuzi? huyo ndiye, Mungu aliyemtuma kuwa mkubwa na mwokozi, awaokoe kwa mkono wa malaika aliyemtokea kichakani.#2 Mose 2:14. 36Kisha huyo akawatoa na kufanya vioja na vielekezo katika nchi ya Misri na katika Bahari Nyekundu, kisha nako jangwani miaka 40.#2 Mose 7:10; 14:21. 37Huyo ndiye yule Mose aliyewaambia wana wa isiraeli: Miongoni mwa ndugu zenu Mungu atawainulia mfumbuaji atakayelingana na mimi.#5 Mose 18:15. 38huyo ndiye aliyekuwa penye wateule jangwani pamoja na yule malaika aliyesema naye mlimani kwa Sinai, tena pamoja na baba zetu. Ndiye aliyepokea maneno ya uzima, atupe sisi;#2 Mose 19:3; Gal. 3:19. 39tena ndiye, ambaye baba zetu hawakutaka kumtii, wakamsukuma, wakageuka mioyoni mwao, kwamba warudi Misri, 40wakamwambia Haroni: Tufanyie miungu itakayotuongoza! Kwani huyo Mose aliyetutoa katika nchi ya Misri hatuyajui yaliyompata.#2 Mose 32:1. 41Siku zile wakatengeneza ndama, nacho kinyago hicho wakakitolea ng'ombe za tambiko, nacho kilichokuwa kazi ya mikono yao wakakishangilia. 42Kisha Mungu akageuka, akawatupa, wavitumikie vikosi vya mbinguni, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Wafumbuaji:
Je? Ng'ombe na vipaji, mlivyovitoa nyikani miaka 40,
vilikuwa vya kunitambikia mimi, ninyi mlio mlango wa
Isiraeli?#Amo. 5:25-27.
43Hapana, ila mlikuwa mmejitwika hema la Moloko
na nyota za mungu wa Romfa;
hivyo vinyago, mlivyovitengeneza,
ndivyo, mlivyovitumia vya kuviangukia.
Kwa hiyo nitawahamisha ninyi, mwende mbali kupita Babeli.
Mambo ya Patakatifu.
44Baba zetu walipokuwa jangwani walikuwa nalo lile Hema la Ushahidi, kama mwenye kusema na Mose alivyoagiza na kumwambia, alitengeneze kwa mfano, aliouona.#2 Mose 25:40. 45Nao baba zetu wakalipokea tena wakiongozwa na Yosua, wakaliingiza katika nchi ya wamizimu, Mungu aliowafukuza mbele ya baba zetu, mpaka siku za Dawidi.#Yos. 3:14; 18:1. 46Huyo akaonea mapendeleo machoni pa Mungu, akaomba ruhusa ya kumpatia Mungu wa Yakobo makazi,#2 Sam. 7:2; Sh. 132:5. 47lakini Salomo ndiye aliyemjengea Nyumba.#1 Fal. 6:1. 48Lakini yeye Alioko huko juu hakai katika nyumba zilizojengwa na mikono ya watu. Ndivyo, anavyosema mfumbuaji:#Yes. 66:1-2.
49Mbingu ni kiti changu cha kifalme, nayo nchi ni pa kuiwekea miguu yangu.
kwa hiyo Bwana anasema:
Ni nyumba gani, mtakayonijengea?
Au mahali pa kupumzikia mimi ni mahali gani?
50Sio mkono wangu ulioyafanya hayo yote?
51Ninyi wenye kosi ngumu, ninyi wenye mioyo na masikio yaliyo kama ya watu wasiotahiriwa, ninyi kila mara humpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu, vivi hivi ninyi nanyi.#2 Mose 32:9; 3 Mose 26:41. 52Ni mfumbuaji gani, ambaye baba zenu hawakumfukuza? Nao walianza kupiga mbiu za kuja kwake huyo Mwongofu waliwaua, tena ni yuleyule, mliyemchongea, kisha mkamwua;#2 Mambo 36:16; Mat. 23:31. 53Maonyo mliyapokea kwa kuagizwa na malaika, lakini hamkuyalinda.#Tume. 7:38; 2 Mose 20; Gal. 3:19; Ebr. 2:2.
Kuuawa kwake Stefano.
54Walipoyasikia haya wakachomwa mioyoni mwao, wakamkerezea meno.#Tume. 5:33. 55Lakini yeye akajaa Roho takatifu, akayaelekeza macho mbinguni akaona utukufu wa Mungu, akamwona naye Yesu, akiwa amesimama kuumeni kwa Mungu, 56akasema: Tazameni, naziona mbingu, zimefunuka, naye Mwana wa mtu amesimama kuumeni kwa Mungu.#Luk. 22:69. 57Ndipo, walipopiga kelele na kupaza sauti na kujiziba masikio, wakamrukia wote pamoja,#3 Mose 24:16; Luk. 23:34,46. 58wakamkumba, atoke mjini, wakampiga mawe. Kulikuwako mashahidi, nao wakazivua nguo zao, wakaziweka miguuni pa kijana, jina lake Sauli,#Tume. 22:20. 59kisha nao wakampiga Stefano mawe, yeye akiomba na kusema: Bwana Yesu, ipokee roho yangu!#Sh. 31:6; Luk. 23:46. 60Kisha akapiga magoti, akaita kwa sauti kuu: Bwana, usiwawekee kosa hili! Alipokwisha kuyasema haya akalala.#Luk. 23:34.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo ya Mitume 7: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia