Mathayo 21
21
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Marko 11:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)
1Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Isa akawatuma wanafunzi wake wawili, 2akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. 3Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.”
4Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema:
5“Mwambieni Binti Sayuni,
‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
ni mpole, naye amepanda punda,
juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’#21:5 Zekaria 9:9”
6Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Isa alivyokuwa amewaagiza. 7Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Isa akaketi juu yake. 8Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani. 9Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema,
“Hosana#21:9 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe., Mwana wa Daudi!”#21:9 Zaburi 118:26
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
“Hosana juu mbinguni!”
10Isa alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”
11Wale umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Isa, yule nabii kutoka Nasiri ya Galilaya.”
Isa atakasa Hekalu
(Marko 11:15-19; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)
12Isa akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’#21:13 Isaya 56:7 lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.”#21:13 Yeremia 7:11
14Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. 15Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.
16Wakamuuliza Isa, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”#21:16 Zaburi 8:2
Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,
“ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya
umeamuru sifa’?”
17Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.
Mtini ulionyauka
(Marko 11:12-14, 20-24)
18Asubuhi na mapema, Isa alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. 19Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.
20Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”
21Isa akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”
Swali kuhusu mamlaka ya Isa
(Marko 11:27-33; Luka 20:1-8)
23Isa alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha, wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka haya?”
24Isa akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 25Je, ubatizo wa Yahya ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”
Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ 26Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yahya kuwa ni nabii.”
27Hivyo basi wakamjibu Isa, “Sisi hatujui.”
Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
Mfano wa wana wawili
28“Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29“Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitaenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.
30“Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine, akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitaenda, bwana,’ lakini hakuenda.
31“Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”
Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”
Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika ufalme wa Mungu. 32Kwa maana Yahya alikuja kwenu kuwaonesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.
Mfano wa wapangaji waovu
(Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)
33“Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo la kukamulia zabibu ndani yake, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri hadi nchi nyingine. 34Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.
35“Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. 36Kisha akawatuma watumishi wengine kwao, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. 37Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
38“Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ 39Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.
40“Basi huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”
41Wakamjibu, “Kwa hasira kuu, atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”
42Isa akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Mwenyezi Mungu ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu’#21:42 Zaburi 118:22, 23?
43“Kwa hiyo ninawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. 44Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”
45Viongozi wa makuhani na Mafarisayo#21:45 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. waliposikia mifano ya Isa, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Isa kuwa ni nabii.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.