Mathayo 20
20
Mfano wa wafanyakazi katika shamba la mizabibu
1“Kwa maana ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri vibarua kufanya kazi katika shamba lake la mizabibu. 2Baada ya kukubaliana na hao vibarua kuwalipa ujira wa dinari#20:2 Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja. moja kwa siku, akawapeleka kwenye shamba lake la mizabibu.
3“Mnamo saa tatu akatoka tena, akawakuta wengine wamesimama sokoni bila kazi. 4Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu, nami nitawalipa chochote kilicho haki yenu.’ 5Hivyo basi wakaenda.
“Akatoka tena mnamo saa sita na pia saa tisa akafanya vivyo hivyo. 6Mnamo saa kumi na moja akatoka tena akawakuta wengine bado wamesimama bila kazi. Akawauliza, ‘Kwa nini mmesimama hapa kutwa nzima pasipo kufanya kazi?’
7“Wakamjibu, ‘Ni kwa sababu hakuna yeyote aliyetuajiri.’
“Akawaambia, ‘Ninyi nanyi nendeni mkafanye kazi katika shamba langu la mizabibu.’
8“Ilipofika jioni, yule mwenye shamba la mizabibu akamwambia msimamizi, ‘Waite hao vibarua na uwalipe ujira wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho na kuishia na wale walioajiriwa kwanza.’
9“Wale vibarua walioajiriwa saa kumi na moja wakaja, na kila mmoja wao akapokea dinari moja. 10Hivyo wale walioajiriwa kwanza walipofika, walidhani watalipwa zaidi. Lakini kila mmoja wao pia alipokea dinari moja. 11Walipoipokea, wakaanza kulalamika dhidi ya yule mwenye shamba, 12wakisema, ‘Hawa watu walioajiriwa mwisho wamefanya kazi kwa muda wa saa moja tu, nawe umewafanya sawa na sisi ambao tumestahimili taabu na joto lote la mchana kutwa?’
13“Yule mwenye shamba akamjibu mmoja wao, ‘Rafiki, sijakudhulumu. Je, hukukubaliana nami kwa ujira wa kawaida wa dinari moja? 14Chukua ujira wako na uende. Mimi nimeamua kumlipa huyu mtu aliyeajiriwa mwisho kama nilivyokupa wewe. 15Je, sina haki ya kufanya kile nitakacho na mali yangu mwenyewe? Au unaona wivu kwa kuwa nimekuwa mkarimu?’
16“Vivyo hivyo, wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.”
Isa atabiri tena kifo chake
(Marko 10:32-34; Luka 18:31-34)
17Basi Isa alipokuwa anapanda kwenda Yerusalemu, aliwaita kando wale wanafunzi kumi na wawili na kuwaambia, 18“Tunapanda kwenda Yerusalemu, na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa viongozi wa makuhani na walimu wa Torati. Nao watamhukumu kifo 19na kumtia mikononi mwa watu wa Mataifa ili wamdhihaki na kumpiga mijeledi na kumsulubisha msalabani. Naye atafufuliwa siku ya tatu!”
Ombi la mama yao Yakobo na Yohana
(Marko 10:35-45)
20Kisha mama yao wana wa Zebedayo akamjia Isa pamoja na wanawe, naye akapiga magoti mbele yake, akamwomba Isa amfanyie jambo fulani.
21Isa akamuuliza, “Unataka nini?” Akajibu, “Tafadhali, wajalie wanangu hawa ili mmoja aketi upande wako wa kuume, na mwingine upande wako wa kushoto katika ufalme wako.”
22Isa akawaambia, “Ninyi hamjui mnaloliomba. Je, mnaweza kukinywea kikombe nitakachonywea mimi?”
Wakajibu, “Tunaweza.”
23Isa akawaambia, “Kwa kweli kikombe changu mtakinywea, lakini kuketi upande wangu wa kuume au wa kushoto si langu mimi kuwapa. Nafasi hizo ni za wale ambao wameandaliwa na Baba#20:23 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu.”
24Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia haya, waliwakasirikia hao ndugu wawili. 25Lakini Isa akawaita wote pamoja na kuwaambia, “Mnafahamu kuwa watawala wa watu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, nao wenye vyeo huonesha mamlaka yao. 26Isiwe hivyo kwenu. Badala yake, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu hana budi kuwa mtumishi wenu, 27naye anayetaka kuwa wa kwanza miongoni mwenu hana budi kuwa mtumwa wenu: 28kama vile Mwana wa Adamu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kuutoa uhai wake uwe fidia kwa ajili ya wengi.”
Isa awaponya vipofu wawili
(Marko 10:46-52; Luka 18:35-43)
29Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakiondoka Yeriko, umati mkubwa wa watu wakamfuata. 30Vipofu wawili walikuwa wameketi kando ya barabara. Waliposikia kwamba Isa alikuwa anapita, wakapaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi#20:30 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4)., tuhurumie!”
31Umati wa watu wakawakemea na kuwaambia wanyamaze, lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema, “Bwana Isa, Mwana wa Daudi, tuhurumie.”
32Isa akasimama na kuwaita, akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”
33Wakamjibu, “Bwana, tunataka kuona.”
34Isa akawahurumia na kuwagusa macho yao. Mara macho yao yakapata kuona, nao wakamfuata.
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 20: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.