Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 19

19
Safari ya kwenda Yerusalemu, na maonyo ya mwisho
(Mathayo 19–23)
Isa afundisha kuhusu talaka
(Marko 10:1-12)
1Isa alipomaliza kusema maneno haya, aliondoka Galilaya, akaenda sehemu za Yudea, ng’ambo ya Yordani. 2Umati mkubwa wa watu wakamfuata, naye akawaponya huko.
3Baadhi ya Mafarisayo#19:3 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakamjia ili kumjaribu, wakamuuliza, “Ni halali mtu kumwacha mke wake kwa sababu yoyote?”
4Akawajibu, “Je, hamkusoma kwamba hapo mwanzo Muumba aliwaumba mwanaume na mwanamke#19:4 Mwanzo 1:27, 5naye akasema, ‘Kwa sababu hii mwanaume atamwacha baba yake na mama yake, naye ataambatana na mkewe, na hao wawili watakuwa mwili mmoja’#19:5 Mwanzo 2:24? 6Hivyo si wawili tena, bali mwili mmoja. Kwa hiyo alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.”
7Wakamuuliza, “Kwa nini basi Musa aliagiza mtu kumpa mkewe hati ya talaka na kumwacha?”
8Isa akawajibu, “Musa aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu. Lakini tangu mwanzo haikuwa hivyo. 9Mimi nawaambia, yeyote amwachaye mkewe isipokuwa kwa sababu ya uasherati naye akaoa mke mwingine, anazini. Naye amwoaye yule mwanamke aliyeachwa pia anazini.”
10Wanafunzi wake wakamwambia, “Kama hali ndiyo hii kati ya mume na mke, ni afadhali mtu asioe!”
11Isa akawaambia, “Si watu wote wanaoweza kupokea neno hili, isipokuwa wale tu waliojaliwa na Mungu. 12Kwa maana wengine ni matowashi kwa sababu wamezaliwa hivyo; wengine wamefanywa matowashi na wanadamu; na wengine wamejifanya matowashi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Yeye awezaye kulipokea neno hili na alipokee.”
Isa awabariki watoto wadogo
(Marko 10:13-16; Luka 18:15-17)
13Kisha watoto wadogo wakaletwa kwa Isa ili aweke mikono yake juu yao na awaombee. Lakini wanafunzi wake wakawakemea wale waliowaleta.
14Isa akasema, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wa wale walio kama hawa.” 15Naye akaweka mikono yake juu yao, na akaondoka huko.
Kijana tajiri
(Marko 10:17-31; Luka 18:18-30)
16Mtu mmoja akamjia Isa na kumuuliza, “Mwalimu mwema, nifanye jambo gani jema ili nipate uzima wa milele?”
17Isa akamjibu, “Mbona unaniuliza habari ya mema? Aliye mwema ni Mmoja tu. Lakini ukitaka kuingia uzimani, zitii amri.”
18Yule mtu akamuuliza, “Amri zipi?”
Isa akamjibu, “Usiue, usizini, usiibe, usishuhudie uongo, 19#19:19 Walawi 19:18waheshimu baba yako na mama yako, na umpende jirani yako kama nafsi yako.”#19:19 Kutoka 20:12-16; Kumbukumbu 5:16-20
20Yule kijana akasema, “Hizi zote nimezishika. Je, bado nimepungukiwa na nini?”
21Isa akamwambia, “Ukitaka kuwa mkamilifu, nenda, ukauze vitu vyote ulivyo navyo, na hizo fedha uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate.”
22Yule kijana aliposikia hayo, akaenda zake kwa huzuni, kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
23Ndipo Isa akawaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambia, itakuwa vigumu kwa mtu tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. 24Tena nawaambia, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko mtu tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
25Wanafunzi wake waliposikia haya, walishangaa sana na kuuliza, “Ni nani basi awezaye kuokoka?”
26Lakini Isa akawatazama, akawaambia, “Kwa mwanadamu jambo hili haliwezekani, lakini mambo yote yanawezekana kwa Mungu.”
27Ndipo Petro akamjibu, “Tazama, sisi tumeacha kila kitu na kukufuata! Tutapata nini basi?”
28Isa akawaambia, “Amin, nawaambia, wakati wa kufanywa upya vitu vyote, Mwana wa Adamu atakapoketi kwenye kiti chake kitukufu cha enzi, ninyi mlionifuata pia mtaketi katika viti kumi na viwili vya utawala, mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli. 29Kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu zake wa kiume au wa kike, baba au mama, watoto au mashamba kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi ya hayo, na ataurithi uzima wa milele. 30Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 19: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia