Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 16

16
Kutambua majira
(Luka 12:54-56)
1Mafarisayo#16:1 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. na Masadukayo#16:1 Kundi la kidini la Wayahudi; waliamini kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho. wakamjia Isa na kumjaribu kwa kumwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.
2Isa akawajibu, “Ifikapo jioni, mnasema, ‘Hali ya hewa itakuwa nzuri, kwa kuwa anga ni nyekundu.’ 3Nanyi wakati wa asubuhi mnasema, ‘Leo kutakuwa na dhoruba, kwa sababu anga ni nyekundu na mawingu yametanda.’ Mnajua jinsi ya kupambanua kule kuonekana kwa anga, lakini hamwezi kupambanua ishara za nyakati. 4Kizazi kiovu na cha uzinzi kinatafuta ishara, lakini hakitapewa ishara yoyote isipokuwa ishara ya Yona.” Isa akawaacha, akaenda zake.
Chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo
(Marko 8:14-21)
5Wanafunzi wake walipofika ng’ambo ya bahari, walikuwa wamesahau kuchukua mikate. 6Isa akawaambia, “Jihadharini. Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na ya Masadukayo.”
7Wakajadiliana wao kwa wao, wakisema, “Ni kwa sababu hatukuleta mikate.”
8Isa, akifahamu majadiliano yao, akauliza, “Enyi wa imani haba! Mbona mnajadiliana miongoni mwenu kuhusu kutokuwa na mikate? 9Je, bado hamwelewi? Je, hamkumbuki ile mikate mitano kwa watu elfu tano, na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya? 10Au ile mikate saba kwa watu elfu nne na idadi ya vikapu vilivyojaa mabaki mlivyokusanya? 11Inakuwaje mnashindwa kuelewa kwamba nilikuwa sisemi nanyi habari za mikate? Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.” 12Ndipo wakaelewa kwamba alikuwa hasemi kuhusu chachu ya kutengeneza mikate, bali kuhusu mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro amkiri Isa kuwa Al-Masihi
(Marko 8:27-30; Luka 9:18-21)
13Basi Isa alipofika katika eneo la Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake, “Watu husema kwamba mimi Mwana wa Adamu ni nani?”
14Wakamjibu, “Baadhi husema ni Yahya; wengine husema ni Ilya; na bado wengine husema ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
15Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”
16Simoni Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Al-Masihi#16:16 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Mwana wa Mungu aliye hai.”
17Naye Isa akamwambia, “Heri wewe, Simoni Bar-Yona#16:17 neno la Kiaramu, maana yake Mwana wa Yona, kwa maana hili halikufunuliwa kwako na mwanadamu, bali na Baba yangu aliye mbinguni. 18Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitajenga jumuiya ya wafuasi wangu, hata malango ya Kuzimu#16:18 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu. hayataweza kuwashinda. 19Nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni, na lolote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa Mbinguni, nalo lolote utakalofungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” 20Kisha akawakataza wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Al-Masihi.
Isa atabiri kifo chake
(Marko 8:31–9:1; Luka 9:22-27)
21Tangu wakati huo, Isa alianza kuwaeleza wanafunzi wake kwamba hana budi kwenda Yerusalemu na kupata mateso mengi mikononi mwa wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa Torati, na kwamba itampasa auawe, lakini siku ya tatu kufufuliwa.
22Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea, akisema, “Haiwezekani, Bwana! Jambo hili kamwe halitakupata!”
23Lakini Isa akageuka na kumwambia Petro, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”
24Ndipo Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate. 25Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayapata. 26Kwa maana itamfaidi mtu nini kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? 27Kwa maana Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, naye ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 28Nawaambia kweli, baadhi yenu hapa hawataonja mauti kabla ya kumwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.”

Iliyochaguliwa sasa

Mathayo 16: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia