Mathayo 17
17
Isa abadilika sura
(Marko 9:2-13; Luka 9:28-36)
1Siku sita baada ya jambo hili, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. 2Wakiwa huko, Isa alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama nuru. 3Ghafula wakawatokea mbele yao Musa na Ilya, wakizungumza na Isa.
4Ndipo Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.”
5Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililong’aa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”
6Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka kifudifudi, wakajawa na hofu. 7Lakini Isa akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” 8Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Isa.
9Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”
10Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
11Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote. 12Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.” 13Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yahya.
Isa amponya kijana mwenye pepo mchafu
(Marko 9:14-29; Luka 9:37-45)
14Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Isa na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15“Bwana#17:15 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”
17Isa akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona tangu saa hiyo.
19Kisha wanafunzi wakamwendea Isa wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
20Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]#17:21 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.”
Isa atabiri kifo chake mara ya pili
22Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. 23Nao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.
Isa na Petro watoa kodi ya Hekalu
24Baada ya Isa na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu#17:24 Kodi hii ilikuwa drakma mbili kwa kila mwanaume; drakma moja ilikuwa na thamani sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”
25Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Isa akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”
26Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.”
Isa akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”
Iliyochaguliwa sasa
Mathayo 17: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.