Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 20

20
Yesu Amefufuka Kutoka Mauti
(Mt 28:1-10; Mk 16:1-8; Lk 24:1-12)
1Asubuhi na mapema siku ya Jumapili, wakati bado lilikuwepo giza, Mariamu Magdalena akaenda kwenye kaburi la Yesu. Naye akaona kuwa lile jiwe kubwa lilikuwa limeondolewa kutoka mlangoni. 2Hivyo akakimbia kwenda kwa Simoni Petro na kwa mfuasi mwingine (yule ambaye Yesu alimpenda sana). Akasema, “Wamemwondoa Bwana kutoka kaburini na hatujui wamemweka wapi.”
3Kwa hiyo Petro na yule mfuasi mwingine wakaanza kuelekea kwenye kaburi. 4Wote walikuwa wakikimbia, lakini yule mfuasi mwingine alikimbia kwa kasi zaidi kuliko Petro na kuwasili wa kwanza kaburini. 5Alipofika akainama chini na kuchungulia ndani ya kaburi. Humo akaviona vipande vya nguo za kitani vikiwa pale chini, lakini hakuingia ndani.
6Hatimaye Simoni Petro akafika kaburini na kuingia ndani. Naye aliviona vipande vile vya nguo za kitani vikiwa chini mle ndani. 7Pia aliiona nguo iliyokuwa imezungushwa kichwani kwa Yesu. Hii ilikuwa imekunjwa na kuwekwa upande mwingine tofauti na pale zilipokuwepo nguo za kitani. 8Kisha mfuasi mwingine, yule aliyefika kwanza kaburini, akaingia ndani. Yeye aliona yaliyotokea na akaamini. 9(Wafuasi hawa walikuwa bado hawajayaelewa yale Maandiko kwamba Yesu alipaswa kufufuka kutoka wafu.)
Yesu Amtokea Mariamu Magdalena
(Mk 16:9-11)
10Kisha wafuasi wakarudi nyumbani. 11Lakini Mariamu akabaki amesimama nje ya kaburi, akilia. Aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi alipokuwa akilia. 12Mle ndani akawaona malaika wawili waliovaa nguo nyeupe na wameketi mahali ulipokuwa mwili wa Yesu. Mmoja amekaa sehemu kilipolazwa kichwa na mwingine aliketi sehemu miguu ilipokuwa imewekwa.
13Malaika wakamwuliza Mariamu, “Mwanamke, kwa nini unalia?”
Mariamu akajibu, “Wameuondoa mwili wa Bwana wangu, na sijui wameuweka wapi.” 14Wakati Mariamu aliposema hivi, akageuka nyuma na kumwona Yesu amesimama pale. Lakini hakujua kuwa huyo alikuwa ni Yesu.
15Akamwuliza, “Mwanamke, kwa nini unalia? Je! unamtafuta nani?”
Yeye alifikiri kuwa huyu alikuwa ni mtunzaji wa bustani. Hivyo akamwambia, “Je! ulimwondoa Bwana? Niambie umemweka wapi. Nami nitaenda kumchukua.” 16Yesu akamwita, “Mariamu.”
Mariamu akamgeukia na kumwambia kwa Kiaramu, “Raboni”, (hii ikiwa na maana “Mwalimu”).
17Yesu akamwambia, “Hupaswi kunishika! Kwani bado sijapaa kwenda huko juu kwa Baba yangu. Lakini nenda ukawaambie wafuasi wangu#20:17 wafuasi wangu Yaani, “ndugu zangu”. maneno haya: ‘Ninarudi kwa Baba yangu ambaye pia ni Baba yenu. Ninarudi kwa Mungu wangu ambaye pia ni Mungu wenu.’”
18Mariamu Magdalena akaenda kwa wafuasi na kuwaambia, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaeleza yale Yesu aliyomwambia.
Yesu Awatokea Wafuasi Wake
(Mt 28:16-20; Mk 16:14-18; Lk 24:36-49)
19Ilikuwa siku ya Jumapili, na jioni ile wafuasi walikuwa pamoja. Nao walikuwa wamefunga milango kwa kuwa waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Ghafla, Yesu akawa amesimama pale katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 20Mara baada ya kusema haya, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Wafuasi walipomwona Bwana, walifurahi sana.
21Kisha Yesu akasema tena, “Amani iwe nanyi. Kama vile Baba alivyonituma, nami sasa nawatuma ninyi vivyo hivyo.” 22Kisha akawapumulia pumzi na kusema, “Pokeeni Roho Mtakatifu. 23Mkisamehe dhambi zake mtu yeyote, dhambi zake hizo zitasamehewa. Kama kuna mtu yeyote ambaye hamtamsamehe dhambi zake, dhambi zake huyo hazitasamehewa.”
Yesu Amtokea Tomaso
24Tomaso (aliyeitwa Pacha) alikuwa ni mmoja wa wale kumi na mbili, lakini hakuwapo pamoja na wafuasi wengine Yesu alipokuja. 25Wakamwambia, “Tulimwona Bwana.” Tomaso akasema, “Hiyo ni ngumu kuamini. Ninahitaji kuona makovu ya misumari katika mikono yake, niweke vidole vyangu ubavuni. Ndipo tu nitakapoamini.” 26Juma moja baadaye wafuasi walikuwemo katika nyumba ile tena, na Tomaso alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja na kusimama katikati yao. Akasema, “Amani iwe nanyi!” 27Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa. Iangalie mikono yangu. Weka mkono wako hapa ubavuni mwangu. Acha kuwa na mashaka na uamini.”
28Tomaso akamwambia Yesu, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29Yesu akamwambia, “Unaamini kwa sababu umeniona. Wana baraka nyingi watu wale wanaoniamini bila kuniona!”
Kwa Nini Yohana Aliandika Kitabu hiki
30Yesu alifanya ishara nyingine nyingi za miujiza ambazo wafuasi wake waliziona, na ambazo hazikuandikwa kwenye kitabu hiki. 31Lakini haya yameandikwa ili muweze kuamini kwamba Yesu ni Masihi, Mwana wa Mungu. Kisha, kwa kuamini, mpate uzima kupitia jina lake.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 20: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia