Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yohana 19

19
1Kisha Pilato akaamuru Yesu aondolewe akachapwe viboko. 2Askari wakatengeneza taji kutokana na matawi yenye miiba na kuiweka kichwani kwake. Kisha wakamzungushia vazi la rangi ya zambarau mwilini mwake. 3Wakaendelea kumkaribia wakisema, “Salamu kwako mfalme wa Wayahudi!” Kisha wakampiga Yesu usoni.
4Kwa mara nyingine Pilato alienda nje na kuwaambia viongozi wa Wayahudi, “Tazameni! Ninamtoa nje Yesu na kumleta kwenu. Ninataka mfahamu kuwa sijapata kwake jambo lolote ambalo kwa hilo naweza kumshitaki.” 5Kisha Yesu akatoka nje akiwa amevishwa taji ya miiba na vazi la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu ndiye mtu mwenyewe!”
6Viongozi wa makuhani na walinzi wa Kiyahudi walipomwona Yesu wakapiga kelele, “Mpigilieni misumari msalabani! Mpigilieni misumari msalabani!”
Lakini Pilato akajibu, “Mchukueni na mpigilieni msalabani ninyi wenyewe. Mimi sioni kosa lolote la kumshitaki.”
7Viongozi wa Wayahudi wakasema, “Tunayo sheria inayosema kuwa ni lazima afe, kwa sababu alisema kuwa yeye ni Mwana wa Mungu.”
8Pilato aliposikia haya, aliogopa zaidi. 9Hivyo akarudi ndani ya jumba lake na kumwuliza Yesu, “Wewe unatoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu kitu. 10Pilato akasema, “Unakataa kusema nami? Kumbuka, ninao uwezo wa kukuweka huru au kukuua msalabani.”
11Yesu akajibu, “Uwezo pekee ulio nao juu yangu ni ule uwezo uliopewa na Mungu. Kwa hiyo yule aliyenitoa mimi kwenu anayo hatia ya dhambi kubwa zaidi.”
12Baada ya hayo, Pilato alijaribu kumwacha huru Yesu. Lakini viongozi wa Wayahudi wakapiga kelele, “Yeyote anayejiweka mwenyewe kuwa mfalme yuko kinyume cha Kaisari. Hivyo kama utamwacha huru mtu huyu, hiyo itakuwa na maana kuwa wewe si rafiki wa Kaisari.”
13Pilato aliposikia maneno hayo, akamtoa nje Yesu na kumweka mahali palipoitwa “Sakafu ya Mawe.” (Kwa Kiaramu jina lake ni Gabatha.) Pale Pilato akaketi katika kiti cha hakimu. 14Wakati huu, ilikuwa imekaribia kuwa saa sita adhuhuri katika Siku ya Matayarisho ya juma la Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”
15Wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Mwue msalabani!”
Pilato akawauliza, “Mnanitaka nimwue mfalme wenu msalabani?”
Viongozi wa makuhani wakajibu, “Kaisari ndiye Mfalme pekee tuliye naye!”
16Hivyo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili auawe juu ya msalaba. Askari wakamchukua Yesu.
Yesu Awambwa Msalabani
(Mt 27:32-44; Mk 15:21-32; Lk 23:26-43)
17Naye Yesu akaubeba msalaba wake hadi mahali panapoitwa “Fuvu la Kichwa”. (Kwa Kiaramu mahali hapo paliitwa “Golgotha”.) 18Hapo wakampigilia Yesu kwa misumari katika msalaba. Pia wakawapigilia kwa misumari watu wengine wawili kwenye misalaba miwili tofauti. Kila mmoja akawekwa pembeni upande wa kushoto na kuume wa msalaba wa Yesu naye akawa katikati yao.
19Pilato akawaambia waandike kibao na kisha kukiweka juu ya msalaba. Kibao hicho kiliandikwa na kilisema, “Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi.” 20Kibao hicho kiliandikwa kwa Kiaramu, Kirumi na Kiyunani. Wayahudi walio wengi walikisoma kibao hicho, kwa sababu mahali ambapo Yesu alipigiliwa kwa misumari msalabani palikuwa karibu na mji.
21Viongozi wa makuhani wa Kiyahudi wakamwambia Pilato, “Usiandike, ‘Mfalme wa Wayahudi.’ Bali andika, ‘Mtu huyu alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.’”
22Pilato akawajibu, “Sitayabadili yale niliyokwisha kuyaandika.”
23Hivyo baada ya askari kumpigilia Yesu kwa misumari msalabani, walizichukua nguo zake na kuzigawa katika mafungu manne. Kila askari alipata fungu moja. Pia wakalichukua vazi lake lililokuwa limefumwa kwa kipande kimoja tu cha kitambaa kutoka juu hadi chini. 24Hivyo askari wakasemezana wao kwa wao, “Hatutalichana vazi hili vipande vipande. Hebu tulipigie kura kuona nani atakayelipata.” Hili lilitokea ili kuweka wazi maana kamili ya yale yanayosemwa katika Maandiko:
“Waligawana miongoni mwao mavazi yangu,
na wakakipigia kura kile nilichokuwa nimevaa.”#Zab 22:18
Hivyo ndivyo maaskari walivyofanya.
25Mama yake Yesu alisimama karibu na msalaba wa mwanawe, Dada yake mamaye Yesu pia alikuwa amesimama pale pamoja na Mariamu mke wake Kleopa, na Mariamu Magdalena. 26Yesu akamwona mama yake na akamwona pia mfuasi aliyempenda sana akisimama pale. Akamwambia mama yake, “Mama mpendwa, mwangalie huyo, naye ni mwanao sasa.” 27Kisha akamwambia yule mfuasi, “Huyu hapa ni mama yako sasa.” Kisha baada ya hayo, mfuasi huyo akamchukua mama yake Yesu na kuishi naye nyumbani kwake.
Yesu Afariki
(Mt 27:45-56; Mk 15:33-41; Lk 23:44-49)
28Baadaye, Yesu akajua kuwa kila kitu kimekwisha kamilika. Ili kuyafanya Maandiko yatimie akasema, “Nina kiu.”#19:28 Nina kiu Tazama Zab 22:15; 69:21. 29Palikuwapo na bakuli lililojaa siki#19:29 siki Divai chungu; yaani, siki ya mvinyo (au divai chungu) uliochanganywa na maji. Hiki kilikuwa kinywaji rahisi na kilichojulikana sana wakati wa Yesu. mahali pale, wale askari wakachovya sponji ndani yake. Wakaiweka ile sponji kwenye tawi la mwanzi na kuliinua hadi kinywani kwa Yesu. 30Alipoionja ile siki, akasema, “Imekwisha.” Baada ya hapo akainamisha kichwa chake na kufa.
31Hii ilikuwa Ijumaa, Siku ya Matayarisho. Siku iliyofuata ilikuwa ni siku ya Sabato maalumu. Viongozi wa Kiyahudi hawakuitaka ile miili ya waliosulubiwa ikae juu misalabani katika siku ya Sabato. Hivyo wakamwomba Pilato atoe amri kuwa miguu ya wale watu misalabani ivunjwe. Pia wakaomba ile miili ishushwe kutoka kwenye misalaba. 32Kwa hiyo askari wakaja na kuivunja miguu#19:32 kuivunja miguu Miguu ilivunjwa ili kuwafanya wale waliokuwa misalabani wafe haraka zaidi. ya watu wale wawili kwenye misalaba kando ya Yesu. 33Lakini askari walipomkaribia Yesu, wakaona kuwa tayari alikuwa amekwisha kufa. Hivyo hawakuivunja miguu yake.
34Lakini mmoja wa askari akauchoma ubavu wa Yesu kwa mkuki wake. Mara hiyo hiyo damu na maji vikamtoka mwilini mwake. 35(Yeye aliyeona haya yakitokea ametueleza. Aliyaeleza haya ili ninyi pia muweze kuamini. Mambo anayosema ni ya kweli. Yeye anajua kuwa anasema kweli.) 36Mambo haya yalitokea ili kutimiza Maandiko yaliyosema, “Hakuna mfupa wake utakaovunjwa”#19:36 Zab 34:20. Wazo linatoka katika Kut 12:46; Hes 9:12. 37na “Watu watamwangalia yeye waliyemchoma.”#Zek 12:10
Yesu Azikwa
(Mt 27:57-61; Mk 15:42-47; Lk 23:50-56)
38Baadaye, mtu mmoja aliyeitwa Yusufu wa kutoka Arimathaya akamwomba Pilato mwili wa Yesu. (Yusufu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini hakumweleza mtu yeyote, kwa sababu aliwaogopa viongozi wa Kiyahudi.) Pilato akasema Yusufu anaweza kuuchukua mwili wa Yesu, hivyo naye akaja na kuuchukua.
39Nikodemu akaenda pamoja na Yusufu. Nikodemu, alikuwa ni yule mtu aliyekuja kwa Yesu hapo kabla na kuzungumza naye usiku. Huyu alileta kadiri ya lita#19:39 lita Kwa maana ya kawaida, “pauni za Kirumi 100” (yaani litras 100), kama kilo 30 hivi. mia moja ya marashi yenye mchanganyiko wa manemane na uvumba. 40Watu hawa wawili wakauchukua mwili wa Yesu na wakauzungushia vipande vya sanda ya kitani pamoja na marashi yale. (Hivi ndivyo Wayahudi walivyowazika watu.) 41Pale msalabani sehemu alipouawa Yesu, palikuwepo na bustani. Katika bustani ile palikuwemo na kaburi#19:41 kaburi Kwa neno “kaburi” hapa inamaanisha ni pango la kuzikia, ambalo siyo shimo tu lililochimbwa ardhini. Pia katika mstari wa 42 na 20:1,2,3,4,6,8 na 11. jipya la kuzikia. Hakuna mtu aliyewahi kuzikwa ndani ya kaburi lile. 42Wanaume wakauweka mwili wa Yesu katika kaburi lile kwa kuwa lilikuwa karibu, na Wayahudi walikuwa wakijiandaa kuianza siku yao ya Sabato.

Iliyochaguliwa sasa

Yohana 19: TKU

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia