Yohana 21
21
Yesu Awatokea wafuasi Wake Saba
1Baadaye, Yesu akawatokea tena wafuasi wake karibu na Ziwa Galilaya. Hivi ndivyo ilivyotokea: 2Baadhi ya wafuasi wake walikuwa pamoja; Simoni Petro, Tomaso (aliyeitwa Pacha), Nathanaeli kutoka Kana kule Galilaya, wana wawili wa Zebedayo, na wafuasi wengine wawili. 3Simoni Petro akasema, “Ninaenda kuvua samaki.”
Wafuasi wengine wakasema, “Sisi sote tutaenda pamoja nawe.” Hivyo wote wakatoka na kwenda kwenye mashua. Usiku ule walivua lakini hawakupata kitu.
4Asubuhi na mapema siku iliyofuata Yesu akasimama ufukweni mwa bahari. Hata hivyo wafuasi wake hawakujua kuwa alikuwa ni yeye Yesu. 5Kisha akawauliza, “Rafiki zangu, mmepata samaki wo wote?”
Wao wakajibu, “Hapana.”
6Yesu akasema, “Tupeni nyavu zenu kwenye maji upande wa kulia wa mashua yenu. Nanyi mtapata samaki huko.” Nao wakafanya hivyo. Wakapata samaki wengi kiasi cha kushindwa kuzivuta nyavu na kuziingiza katika mashua.
7Mfuasi aliyependwa sana na Yesu akamwambia Petro, “Mtu huyo ni Bwana!” Petro aliposikia akisema kuwa alikuwa Bwana, akajifunga joho lake kiunoni. (Alikuwa amezivua nguo zake kwa vile alitaka kufanya kazi.) Ndipo akaruka majini. 8Wafuasi wengine wakaenda ufukweni katika mashua. Wakazivuta nyavu zilizojaa samaki. Nao hawakuwa mbali sana na ufukwe, walikuwa kadiri ya mita 100#21:8 mita 100 Au “mikono 200”. tu. 9Walipotoka kwenye mashua na kuingia kwenye maji, wakaona moto wenye makaa yaliokolea sana. Ndani ya moto huo walikuwemo samaki na mikate pia. 10Kisha Yesu akasema leteni baadhi ya samaki mliowavua.
11Simoni Petro akaenda kwenye mashua na kuvuta wavu kuelekea ufukweni. Wavu huo ulikuwa umejaa samaki wakubwa, wapatao 153 kwa ujumla! Lakini pamoja na wingi wa samaki hao, nyavu hazikukatika. 12Yesu akawaambia, “Njooni mle.” Hakuna hata mfuasi mmoja aliyemwuliza, “Wewe ni nani?” Walijua yeye alikuwa ni Bwana. 13Yesu akatembea ili kuchukua mikate na kuwapa. Akawapa samaki pia.
14Hii sasa ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
Yesu Azungumza na Petro
15Walipomaliza kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, “Simoni, mwana wa Yohana, je, unanipenda kuliko watu wote hawa wanavyonipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akamwambia, “Wachunge wanakondoo#21:15 wanakondoo Yesu alitumia neno hili au neno “kondoo” katika mistari 16 na 17 ikimaanisha wafuasi wake, kama ilivyo katika Yh 10. wangu.”
16Kwa mara nyingine Yesu akamwambia, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akajibu, “Ndiyo, Bwana, wewe unajua kuwa nakupenda.”
Kisha Yesu akasema, “Watunze kondoo wangu.”
17Mara ya tatu Yesu akasema, “Simoni, mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika kwa sababu Yesu alimuuliza mara tatu, “Unanipenda?” Akasema, “Bwana, unafahamu kila kitu. Unajua kuwa nakupenda!”
Yesu akamwambia, “Walinde kondoo wangu. 18Ukweli ni huu, wakati ulipokuwa mdogo, ulijifunga mwenyewe mkanda wako kiunoni na kwenda ulikotaka. Lakini utakapozeeka, utainyoosha mikono yako,#21:18 utainyoosha mikono yako Kunyoosha mikono ilikuwa no njia ya kawaida ya kusema juu ya kusulubishwa. na mtu mwingine atakufunga mkanda wako. Watakuongoza kwenda mahali usikotaka kwenda.” 19(Yesu alisema hivi kumwonyesha jinsi Petro atakavyokufa ili kumpa utukufu Mungu.) Kisha akamwambia Petro, “Nifuate!”
20Petro akageuka na kumwona yule mfuasi mwingine aliyependwa sana na Yesu akitembea nyuma yao. (Huyu alikuwa ni mfuasi aliyejilaza kwa Yesu wakati wa chakula cha jioni na kusema, “Bwana, ni nani atakayekusaliti kwa maadui zako?”) 21Petro alipomwona nyuma yao, akamwuliza Yesu, “Bwana, vipi kuhusu yeye?”
22Yesu akajibu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali. Wewe nifuate!”
23Kwa hiyo habari ikaenea miongoni mwa wafuasi wa Yesu. Wao walikuwa wakisema kuwa mfuasi huyo asingekufa. Lakini Yesu hakusema kuwa asingekufa. Yeye alisema tu, “Labda nataka awe hai hadi nitakaporudi. Hilo wewe usilijali.”
24Huyo mfuasi ndiye yeye anayesimulia habari hizi. Ndiye ambaye sasa ameziandika habari zote hizi. Nasi tunajua kuwa anayoyasema ni kweli.
25Kuna mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu. Kama kila moja ya hayo yote yangeandikwa, nafikiri ulimwengu wote usingevitosha vitabu ambavyo vingeandikwa.
Iliyochaguliwa sasa
Yohana 21: TKU
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili
![None](/_next/image?url=https%3A%2F%2Fimageproxy.youversionapi.com%2F58%2Fhttps%3A%2F%2Fweb-assets.youversion.com%2Fapp-icons%2Fsw.png&w=128&q=75)
Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International