Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 19

19
Yesu na Zakayo#19:1-10 Kisa hiki kinasimuliwa na Luka peke yake nacho chaonesha tena jinsi Yesu anavyojihusisha na watu wanaodharauliwa na viongozi wa dini. Uamuzi wake alipokumbana na Yesu ni kinyume kabisa na kile kisa cha tajiri (18:18-23).
1Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa akipita katika njia za mji huo. 2Palikuwa na mtu mmoja huko mjini aitwaye Zakayo#19:2 Zakayo: Kwa vile alikuwa mkuu au kiongozi wa watozaushuru wilayani humo, alikuwa amejipatia nafasi nyingi za kuweza kuwa tajiri kutokana na fedha zisizo halali (aya 8). ambaye alikuwa mkuu wa watozaushuru, na pia mtu tajiri. 3Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu. 4Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu#19:4 Mkuyu: Neno kwa neno sikamoro; mti wa jamii ya mtini, mkubwa na wenye matawi mengi na ambao ulikuwa rahisi kupanda juu yake. ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo. 5Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako.” 6Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha. 7Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung'unika wakisema, “Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi.” 8Lakini Zakayo akasimama, akamwambia Yesu, “Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang'anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne.”#19:8 Nitamrudishia mara nne: Zakayo anafanya hata zaidi ya yale yaliyotakiwa na sheria ya Mose (Lawi 6:1-5; Hes 5:5-7). 9Yesu akamwambia, “Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.#19:9 Wa ukoo wa Abrahamu: Yaani Myahudi halisi, mmoja wa watu wa Mungu. 10Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea.”
Mfano wa watumishi kumi#19:11-27 Mfano huu unafanana na ule wa Mat 25:14-20 na unafundisha kama huo wa Mathayo umuhimu wa wafuasi wa Yesu kuwajibika kuhusu vitu walivyokabidhiwa. Lakini mfano huu wa Luka unaweka fundisho lingine: Bwana huyo atakaporudi kama mfalme anaamuru maadui zako wauawe.
(Mat 25:14-30)
11Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, ufalme wa Mungu ungefika. 12Hivyo akawaambia, “Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.#19:12 Wafalme na watawala wa Palestina waliwekwa na Kaisari, mfalme wa Roma. Yawezekana kwamba mfano huu wagusia safari aliyoifanya Arkelao kwenda Roma mwaka wa 4 K.K. kuthibitishwa katika wadhifa wa mkuu wa mkoa au gavana; baadhi ya Wayahudi walimfuata huko kupinga kuteuliwa kwake, (ling na aya 4). 13Basi, kabla ya kuondoka, aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha#19:13 Kiasi cha fedha: Neno kwa neno: mia moja, au kiasi cha fedha kadiri ya mshahara ambao kawaida alipewa mtu kwa kazi ya siku mia moja, au dinari 100. kila mmoja na kuwaambia: ‘Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.’ 14Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: ‘Hatumtaki huyu atutawale.’
15“Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani. 16Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.’ 17Naye akamwambia: ‘Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!’ 18Mtumishi wa pili akaja, akasema: ‘Bwana, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.’ 19Naye akamwambia pia: ‘Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.’
20“Mtumishi mwingine akaja, akasema: ‘Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa, 21kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na kuchuma ambacho hukupanda.’ 22Naye akamwambia: ‘Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda. 23Kwa nini, basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?’ 24Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: ‘Mnyang'anyeni hiyo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.’ 25Nao wakamwambia: ‘Lakini Bwana, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!’ 26Naye akawajibu: ‘Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa. 27Na sasa, kuhusu hao maadui zangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu.’”
Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mat 21:1-11; Marko 11:1-11; Yoh 12:12-19)
28Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.#19:28-44 Kwa namna yake ya kuingia Yerusalemu, Yesu anaonesha kwa ishara kwamba yeye ndiye Masiha au Mwokozi aliyetumwa na Mungu (linganisha Zek 9:9). Sehemu ya aya 45-48, inaonesha uwezo na mamlaka yake ya kimasiha kwa ishara nyingine ya mfano. 29Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni,#19:29 Bethfage …Bethania … Mizeituni: Mahali penyewe panapotajwa ni karibu na Yerusalemu, yapata kilomita moja kutoka mjini. aliwatuma wanafunzi wake wawili, 30akawaambia: “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwanapunda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungueni, mkamlete hapa. 31Kama mtu akiwauliza kwa nini mnamfungua, mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’”
32Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. 33Walipokuwa wanamfungua yule mwanapunda, wenyewe wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua mwanapunda huyu?” 34Nao wakawajibu, “Bwana anamhitaji.” 35Basi, wakampelekea Yesu yule mwanapunda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake, wakampandisha Yesu juu yake.#19:35 Ling na Zek 9:9. 36Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani.#19:36 Wakatandaza mavazi yao barabarani: Hivyo vilikuwa vitendo vilivyoonesha makaribisho (taz 2Fal 9:13).
37Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; 38wakawa wanasema: “Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana.#19:38 Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana: Zab 118:26, makala ambayo ilitumiwa kuwasalimu mahujaji. Awali maneno hayo yalitumiwa kumsalimu mfalme wakati alipokwenda hekaluni, na hapa ni muhimu kwamba watu wanayataja maneno hayo kuhusu kuwasili kwake Yesu. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!”
39Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu wakamwambia Yesu, “Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!” 40Yesu akawajibu, “Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti.”
Yesu anauombolezea Yerusalemu
41Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia 42akisema: “Laiti ungelijua leo hii mambo yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. 43Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote.#19:43-44 Namna ya kusema na lugha inayofanana na Isa 29:3; Yer 6:6; Eze 4:2. Mwaka 70 K.K. kikosi cha jeshi la Kiroma kiliteketeza Yerusalemu. Ling na Luka 21:6,20-24. 44Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia#19:44 Mungu alipokujia: Katika Kigiriki na pia Kiebrania neno kutembelea au kumjia mtu linatumiwa kutaja kuhusika kwa Mungu, au hatua anayochukua Mungu kuokoa (taz maelezo ya Luka 1:69), au kuadhibu (Kut 20:5; 32:34; Zab 59:5; Isa 10:12). kukuokoa.”
Yesu anaingia hekaluni
(Mat 21:12-17; Marko 11:15-19; Yoh 2:13-22)
45Kisha, Yesu aliingia hekaluni, akaanza kuwafukuza nje wafanyabiashara 46akisema, “Imeandikwa: ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala’; lakini nyinyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.”#19:46 Wanyang'anyi: Ling na Isa 56:7; Yer 7:11.
47Yesu akawa anafundisha kila siku hekaluni. Makuhani wakuu, waalimu wa sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, 48lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.

Iliyochaguliwa sasa

Luka 19: BHNTLK

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia