Ruthu 2:1-18
Ruthu 2:1-18 SRUV
Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Niruhusu niende shambani, niokote mabaki ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota mabaki shambani nyuma ya wavunaji; na kwa bahati akafikia sehemu ya shamba la Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu na kuwaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota mabaki, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hadi sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. Basi Ruthu akaokota mabaki shambani hadi jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa.