Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Rut 2:1-18

Rut 2:1-18 SUV

Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. Basi Ruthu akaokota masazo kondeni hata jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonyesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa.

Soma Rut 2