Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 2

2
Ruthu akutana na Boazi
1 # Rut 3:2,12 Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. 2#Law 19:9-10; 23:22; Kum 24:19 Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Niruhusu niende shambani, niokote mabaki ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. 3Basi akaenda, akaja akaokota mabaki shambani nyuma ya wavunaji; na kwa bahati akafikia sehemu ya shamba la Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. 4#Amu 6:12; Zab 118:26; 129:7,8; Lk 1:28; 2 The 3:16; 2 Tim 4:22; Kol 4:6 Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu na kuwaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. 5Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? 6#Rut 1:22 Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; 7naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota mabaki, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hadi sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo.
8Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. 9Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. 10#Mwa 18:2; 1 Sam 25:23 Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? 11#Mit 31:31; Rut 1:14; Lk 5:11,28; 14:33; 18:29,30; Ebr 11:8,9,24-26 Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. 12#1 Sam 24:19; Zab 19:11; 58:11; Mit 11:18; Mt 5:12; 6:1; Lk 6:35; 14:12-14; 2 Tim 1:18; Ebr 6:10; 11:6,26; Zab 17:8; 36:7 BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. 13#1 Sam 25:41; Flp 2:3 Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako.
14Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. 15Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. 16Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. 17Basi Ruthu akaokota mabaki shambani hadi jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. 18Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa.
19Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. 20#Law 25:25; Rut 3:10; 2 Sam 2:5; Ayu 29:13; 2 Tim 1:16; Mit 17:17; Rut 3:9; 4:6 Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na BWANA, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwa waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa ukoo wetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. 21Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na watumishi wangu, hadi watakapomaliza mavuno yangu yote. 22Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, ili watu wasikusumbue katika shamba lingine lolote lile. 23Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.

Iliyochaguliwa sasa

Ruthu 2: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia