Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 35:1-28

Zaburi 35:1-28 SRUV

Ee BWANA, uwapinge hao wanaonipinga, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kikingio, Uinuke unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibike na kufedheheka, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafla, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini kutoka kwa mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye. Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nilijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nilisikitika kana kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Niliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa wanafurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wakanipapura bila kukoma. Bila heshima walinidhihaki kupindukia, Wakanisagia meno yao. BWANA, utatazama hadi lini? Uiokoe nafsi yangu kutoka kwa maangamizi yao, Na maisha yangu kutoka kwa wanasimba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi. Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e. Maana hawasemi maneno ya amani, Ila juu ya watulivu wa nchi huwaza hila. Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona. Wewe, BWANA, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami. Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu. Unihukumu kwa haki yako, Ee BWANA, Mungu wangu, Na usiwaache wanisimange. Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza. Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu. Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe BWANA, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake. Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.

Soma Zaburi 35

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zaburi 35:1-28

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha