Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 35:1-28

Zaburi 35:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Ee Mwenyezi-Mungu, uwapinge hao wanaonipinga; uwashambulie hao wanaonishambulia. Utwae ngao yako na kingio lako, uinuke uje ukanisaidie! Chukua mkuki na sime yako dhidi ya wanaonifuatia. Niambie mimi kwamba utaniokoa. Waone haya na kuaibika, hao wanaoyanyemelea maisha yangu! Warudishwe nyuma kwa aibu, hao wanaozua mabaya dhidi yangu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, wakikimbizwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Njia yao iwe ya giza na utelezi, wakifukuzwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu! Maana walinitegea mitego bila sababu; walinichimbia shimo bila kisa chochote. Maangamizi yawapate wao kwa ghafla, wanaswe katika mtego wao wenyewe, watumbukie humo na kuangamia! Hapo mimi nitafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu; nitashangilia kwa kuwa yeye ameniokoa. Nitamwambia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote: “Wewe ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe! Wewe wawaokoa wanyonge makuchani mwa wenye nguvu, maskini na fukara mikononi mwa wanyanganyi.” Mashahidi wakorofi wanajitokeza; wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mema yangu kwa mabaya; nami binafsi nimebaki katika ukiwa. Lakini wao walipokuwa wagonjwa, mimi nilivaa magunia kuonesha huzuni; nilijitesa kwa kujinyima chakula. Nilisali nikiwa nimeinamisha kichwa, kana kwamba namlilia rafiki au ndugu yangu. Nilikwenda huko na huko kwa huzuni, kama mtu anayeomboleza kifo cha mama yake. Lakini mimi nilipoanguka walikusanyika kunisimanga. Walikusanyika pamoja dhidi yangu. Watu nisiowajua walinirarua bila kukoma, wala hakuna aliyewazuia. Watu ambao huwadhihaki vilema, walinisagia meno yao kwa chuki. Ee Mwenyezi-Mungu, utatazama tu mpaka lini? Uniokoe kutoka kwenye mashambulio yao; uyaokoe maisha yangu na simba hao. Hapo nitakushukuru kati ya kusanyiko kubwa la watu; nitakutukuza kati ya jumuiya kubwa ya watu. Usiwaache maadui hao wabaya wanisimange, hao wanichukiao bure wafurahie mateso yangu. Maneno wasemayo si ya amani, wanazua maneno ya hila dhidi ya wananchi watulivu. Wananishtaki kwa sauti: “Haya! Haya! Tumeona wenyewe uliyotenda!” Lakini wewe Mwenyezi-Mungu waona jambo hilo, usinyamaze, ee Mwenyezi-Mungu, usikae mbali nami. Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukanitetee; uje, ee Mungu wangu, uangalie kisa changu. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, unitetee, ufanye kulingana na uadilifu wako; usiwaache maadui zangu wanisimange. Usiwaache wajisemee: “Tumefanikiwa tulivyotaka!” Au waseme: “Tumemmaliza huyu!” Waache hao wanaofurahia maafa yangu, washindwe wote na kufedheheka. Hao wote wanaojiona wema kuliko mimi, waone haya na kuaibika. Lakini wanaotaka kuona kuwa sina hatia, wapaaze sauti kwa furaha waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni mkuu mno! Hupendezwa na fanaka ya mtumishi wake.” Hapo nami nitatangaza uadilifu wako; nitasema sifa zako mchana kutwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 35

Zaburi 35:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ee BWANA, uwapinge hao wanaonipinga, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kikingio, Uinuke unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibike na kufedheheka, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafla, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini kutoka kwa mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye. Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nilijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nilisikitika kana kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Niliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa wanafurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wakanipapura bila kukoma. Bila heshima walinidhihaki kupindukia, Wakanisagia meno yao. BWANA, utatazama hadi lini? Uiokoe nafsi yangu kutoka kwa maangamizi yao, Na maisha yangu kutoka kwa wanasimba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi. Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining'ong'e. Maana hawasemi maneno ya amani, Ila juu ya watulivu wa nchi huwaza hila. Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona. Wewe, BWANA, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami. Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu. Unihukumu kwa haki yako, Ee BWANA, Mungu wangu, Na usiwaache wanisimange. Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza. Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu. Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe BWANA, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake. Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 35

Zaburi 35:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ee BWANA, utete nao wanaoteta nami, Upigane nao wanaopigana nami. Uishike ngao na kigao, Usimame unisaidie. Uutoe na mkuki uwapinge wanaonifuatia, Uiambie nafsi yangu, Mimi ni wokovu wako. Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini. Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia. Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake. Na nafsi yangu itamfurahia BWANA, Na kuushangilia wokovu wake. Mifupa yangu yote itasema, BWANA, ni nani aliye kama Wewe? Umponyaye maskini na mtu aliye hodari kumshinda yeye, Naam, maskini na mhitaji na mtu amtekaye. Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi. Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno. BWANA, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi. Walio adui zangu bure wasinisimange, Wanaonichukia bila sababu wasining’ong’e. Maana hawasemi maneno ya amani, Na juu ya watulivu wa nchi huwaza hila. Nao wananifumbulia vinywa vyao, Husema, Ewe! Ewe! Jicho letu limeona. Wewe, BWANA, umeona, usinyamaze; Ee Bwana, usiwe mbali nami. Uamke, uwe macho ili kunipatia hukumu Kwa ajili ya madai yangu, Mungu wangu na Bwana wangu. Unihukumu kwa haki yako, Ee BWANA, Mungu wangu, Wala wasinisimangize. Wasiseme moyoni, Haya! Ndivyo tutakavyo; Wasiseme, Tumemmeza. Waaibishwe, wafedheheshwe pamoja, Wanaoifurahia hali yangu mbaya. Wavikwe aibu na fedheha, Wanaojikuza juu yangu. Washangilie na kufurahi, Wapendezwao na haki yangu. Naam, waseme daima, Atukuzwe BWANA, Apendezwaye na amani ya mtumishi wake. Na ulimi wangu utanena haki yako, Na sifa zako mchana kutwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 35

Zaburi 35:1-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Ee BWANA, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami. Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie. Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.” Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu. Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa BWANA akiwafukuza. Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa BWANA akiwafuatilia. Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo, maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao. Ndipo nafsi yangu itashangilia katika BWANA na kuufurahia wokovu wake. Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee BWANA? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!” Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa. Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia na nikajinyenyekesha kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa, niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu. Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma. Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno. Ee BWANA, utatazama mpaka lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa. Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi. Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila. Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi. Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.” Ee BWANA, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee BWANA. Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu. Nihukumu kwa haki yako, Ee BWANA Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange. Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.” Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau. Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “BWANA atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.” Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.

Shirikisha
Soma Zaburi 35

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha