Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 35

35
Kuomba msaada
(Zaburi ya Daudi)
1Ee Mwenyezi-Mungu, uwapinge hao wanaonipinga;
uwashambulie hao wanaonishambulia.
2Utwae ngao yako na kingio lako,
uinuke uje ukanisaidie!
3Chukua mkuki na sime yako dhidi ya wanaonifuatia.
Niambie mimi kwamba utaniokoa.
4Waone haya na kuaibika,
hao wanaoyanyemelea maisha yangu!
Warudishwe nyuma kwa aibu,
hao wanaozua mabaya dhidi yangu.
5Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo,
wakikimbizwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu!
6Njia yao iwe ya giza na utelezi,
wakifukuzwa na malaika wa Mwenyezi-Mungu!
7Maana walinitegea mitego bila sababu;
walinichimbia shimo bila kisa chochote.
8Maangamizi yawapate wao kwa ghafla,
wanaswe katika mtego wao wenyewe,
watumbukie humo na kuangamia!
9Hapo mimi nitafurahi kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu;
nitashangilia kwa kuwa yeye ameniokoa.
10Nitamwambia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wangu wote:
“Wewe ee Mwenyezi-Mungu, hakuna aliye kama wewe!
Wewe wawaokoa wanyonge makuchani mwa wenye nguvu,
maskini na fukara mikononi mwa wanyanganyi.”
11Mashahidi wakorofi wanajitokeza;
wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12Wananilipa mema yangu kwa mabaya;
nami binafsi nimebaki katika ukiwa.
13Lakini wao walipokuwa wagonjwa,
mimi nilivaa magunia kuonesha huzuni;
nilijitesa kwa kujinyima chakula.
Nilisali nikiwa nimeinamisha kichwa,
14kana kwamba namlilia rafiki au ndugu yangu.
Nilikwenda huko na huko kwa huzuni,
kama mtu anayeomboleza kifo cha mama yake.
15Lakini mimi nilipoanguka walikusanyika kunisimanga.
Walikusanyika pamoja dhidi yangu.
Watu nisiowajua walinirarua bila kukoma,
wala hakuna aliyewazuia.
16Watu ambao huwadhihaki vilema,
walinisagia meno yao kwa chuki.
17Ee Mwenyezi-Mungu, utatazama tu mpaka lini?
Uniokoe kutoka kwenye mashambulio yao;
uyaokoe maisha yangu na simba hao.
18Hapo nitakushukuru kati ya kusanyiko kubwa la watu;
nitakutukuza kati ya jumuiya kubwa ya watu.
19 # Taz Zab 69:4; Yoh 15:25 Usiwaache maadui hao wabaya wanisimange,
hao wanichukiao bure wafurahie mateso yangu.
20Maneno wasemayo si ya amani,
wanazua maneno ya hila dhidi ya wananchi watulivu.
21Wananishtaki kwa sauti:
“Haya! Haya! Tumeona wenyewe uliyotenda!”
22Lakini wewe Mwenyezi-Mungu waona jambo hilo,
usinyamaze, ee Mwenyezi-Mungu,
usikae mbali nami.
23Uinuke, ee Mwenyezi-Mungu, ukanitetee;
uje, ee Mungu wangu, uangalie kisa changu.
24Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, unitetee,
ufanye kulingana na uadilifu wako;
usiwaache maadui zangu wanisimange.
25Usiwaache wajisemee: “Tumefanikiwa tulivyotaka!”
Au waseme: “Tumemmaliza huyu!”
26Waache hao wanaofurahia maafa yangu,
washindwe wote na kufedheheka.
Hao wote wanaojiona wema kuliko mimi,
waone haya na kuaibika.
27Lakini wanaotaka kuona kuwa sina hatia,
wapaaze sauti kwa furaha waseme daima:
“Mwenyezi-Mungu ni mkuu mno!
Hupendezwa na fanaka ya mtumishi wake.”
28Hapo nami nitatangaza uadilifu wako;
nitasema sifa zako mchana kutwa.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 35: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha