Zaburi 140:1-13
Zaburi 140:1-13 SRUV
Ee BWANA, uniokoe kutoka kwa watu waovu. Unihifadhi kutoka kwa watu wajeuri. Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huchochea vita. Wamenoa ndimi zao na kuwa kama za nyoka, Na katika midomo yao mna sumu ya fira. Ee BWANA, unilinde Kutoka kwa mikono ya mtu asiye haki; Unihifadhi na watu wajeuri; Waliopanga kuniangusha. Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando ya njia; Wameniwekea matanzi. Nimemwambia BWANA, Ndiwe Mungu wangu; Ee BWANA, uisikie sauti ya dua zangu. Ee MUNGU Bwana, nguvu za wokovu wangu, Umenifunika kichwa changu siku ya vita. Ee BWANA, usimpe asiye haki tamaa zake, Usiifanikishe hila yake, wasije wakajiinua. Nao wainuapo vichwa watu wanaonizunguka, Madhara ya midomo yao yawafunike. Makaa ya moto yawaangukie, watupwe motoni, Na katika mashimo, wasipate kusimama tena. Msingiziaji hatawekwa imara katika nchi, Mtu wa jeuri, uovu humwinda kumwangamiza. Najua ya kuwa BWANA atamfanyia mnyonge hukumu, Na wahitaji haki yao. Hakika wenye haki watalishukuru jina lako, Wenye adili watakaa mahali ulipo Wewe.