Zaburi 103:15-22
Zaburi 103:15-22 SRUV
Mwanadamu siku zake zi kama majani; Kama ua la kondeni ndivyo anavyostawi. Maana upepo hupita juu yake, na kutoweka! Lisionekane mahali lilipokuwa tena. Bali fadhili za BWANA ni kwa wamchao Tangu milele hata milele, Na haki yake ni kwa vizazi vyote; Kwa wale walishikao agano lake, Na kuyakumbuka maagizo yake ili wayafanye. BWANA ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, Na ufalme wake unavitawala vitu vyote. Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake. Mhimidini BWANA, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake. Mhimidini BWANA, enyi matendo yake yote, Mahali pote pa milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA.