Mithali 28:15-28
Mithali 28:15-28 SRUV
Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini. Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake. Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie. Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara. Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha. Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa. Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate. Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjia. Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake. Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu. Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye BWANA ataneemeshwa. Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa. Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi. Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.