Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 28:15-28

Mithali 28:15-28 NENO

Kama simba angurumaye au dubu ashambuliaye, ndivyo alivyo mtu mwovu anayetawala wanyonge. Mtawala dhalimu hana akili, bali yeye achukiaye mapato ya udhalimu atafurahia maisha marefu. Mtu mwenye kusumbuliwa na hatia ya kuua atakuwa mtoro hadi kufa; mtu yeyote asimsaidie. Yeye ambaye mwenendo wake hauna lawama hulindwa salama, bali yeye ambaye njia zake ni potovu ataanguka ghafula. Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele, bali yule afuataye mambo ya upuzi atakuwa na umaskini wa kumtosha. Mtu mwaminifu atabarikiwa sana, bali yeye atamaniye kupata utajiri kwa haraka hataacha kuadhibiwa. Kuonesha upendeleo si vizuri, hata hivyo mtu atafanya kosa kwa kipande cha mkate. Mtu mchoyo ana tamaa ya kupata utajiri, naye hana habari kuwa umaskini unamngojea. Yeye amkemeaye mtu mwishoni hupata kibali zaidi, kuliko mwenye maneno ya kusifu isivyostahili. Yeye amwibiaye babaye au mamaye na kusema, “Si kosa,” yeye ni mwenzi wa yule aharibuye. Mtu mwenye tamaa huchochea fitina, bali yule amtegemeaye Mwenyezi Mungu atafanikiwa. Yeye ajitumainiaye mwenyewe ni mpumbavu, bali yeye atembeaye katika hekima hulindwa salama. Yeye ampaye maskini hatapungukiwa na kitu chochote, bali yeye awafumbiaye maskini macho hupata laana nyingi. Wakati waovu wanatawala, watu huenda mafichoni, bali waovu wanapoangamia, wenye haki hufanikiwa.