Mathayo 5:33-48
Mathayo 5:33-48 SRUV
Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana viapo vyako; lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa nchi, kwa maana ndipo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu. Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kulia, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kulichukua shati lako, mwachie na koti pia. Mtu yeyote akikulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye maili mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo. Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mnapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi sawa na hayo? Basi ninyi iweni wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.