Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 5:33-48

Mathayo 5:33-48 Biblia Habari Njema (BHN)

“Tena mmesikia kwamba watu wa kale waliambiwa: ‘Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana.’ Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, ‘Ndiyo’, basi iwe ‘Ndiyo’; ukisema, ‘Siyo’, basi iwe kweli ‘Siyo’. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu. “Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Jicho kwa jicho, jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia la pili. Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. Mtu akikulazimisha kubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili. Akuombaye mpe, wala usimpe kisogo anayetaka kukukopa kitu. “Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘Mpende jirani yako, na kumchukia adui yako.’ Lakini mimi nawaambieni, wapendeni maadui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyinyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu wabaya na wema, na kuwanyeshea mvua watu wanyofu na waovu. Je, mtapata tuzo gani kwa kuwapenda tu wale wanaowapenda nyinyi? Hakuna! Kwa maana, hata watozaushuru hufanya hivyo! Kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mmefanya kitu kisicho cha kawaida? Hata watu wasiomjua Mungu nao hufanya vivyo hivyo. Basi, muwe wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Shirikisha
Soma Mathayo 5

Mathayo 5:33-48 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

“Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. Mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. Mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu, na waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? Nanyi mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu hawafanyi hivyo? Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

Shirikisha
Soma Mathayo 5