Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mathayo 5:33-48

Mathayo 5:33-48 NEN

“Tena mmesikia walivyoambiwa watu wa zamani kwamba, ‘Usiape kwa uongo, bali timiza kiapo kile ulichofanya kwa Bwana.’ Lakini mimi nawaambia, msiape kabisa: iwe kwa mbingu, kwa kuwa ni kiti cha enzi cha Mungu; au kwa dunia, kwa kuwa ndipo mahali pake pa kuwekea miguu; au kwa Yerusalemu, kwa kuwa ndio mji wa Mfalme Mkuu. Nanyi msiape kwa vichwa vyenu, kwa kuwa hamwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. ‘Ndiyo’ yenu iwe ‘Ndiyo,’ na ‘Hapana’ yenu iwe ‘Hapana.’ Lolote zaidi ya hili latoka kwa yule mwovu. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Jicho kwa jicho na jino kwa jino.’ Lakini mimi nawaambia, msishindane na mtu mwovu. Lakini kama mtu akikupiga kwenye shavu la kuume, mgeuzie na la pili pia. Kama mtu akitaka kukushtaki na kuchukua joho lako, mwachie achukue na koti pia. Kama mtu akikulazimisha kwenda maili moja, nenda naye maili mbili. Mpe yeye akuombaye, wala usimgeuzie kisogo yeye atakaye kukukopa. “Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ Lakini ninawaambia: Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo? Nanyi kama mkiwasalimu ndugu zenu tu, je, mnafanya nini zaidi ya wengine? Je, hata watu wasiomjua Mungu, hawafanyi hivyo? Kwa hiyo kuweni wakamilifu kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.