Luka 23:26-38
Luka 23:26-38 SRUV
Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shambani, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu. Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu. Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha. Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni. Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu? Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye. Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulubisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kulia, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura. Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake. Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki, huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe. Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.