Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:26-38

Luka 23:26-38 Biblia Habari Njema (BHN)

Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: ‘Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!’ Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: ‘Tuangukieni!’ Na vilima, ‘Tufunikeni!’ Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?” Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!” Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”

Shirikisha
Soma Luka 23

Luka 23:26-38 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu. Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ Ndipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!” ’ Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?” Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulubiwe. Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura. Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.” Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.

Shirikisha
Soma Luka 23