Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Luka 23:26-38

Luka 23:26-38 NEN

Walipokuwa wakienda naye, wakamkamata mtu mmoja aitwaye Simoni mwenyeji wa Kirene, aliyekuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shambani. Wakambebesha msalaba, wakamlazimisha auchukue nyuma ya Yesu. Idadi kubwa ya watu wakamfuata Yesu, wakiwamo wanawake waliokuwa wakimlilia na kumwombolezea. Yesu akawageukia, akawaambia, “Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi bali jililieni ninyi wenyewe na watoto wenu. Kwa maana wakati utafika mtakaposema, ‘Wamebarikiwa wanawake tasa, ambao matumbo yao hayakuzaa, wala matiti yao hayakunyonyesha!’ Ndipo “ ‘wataiambia milima, “Tuangukieni!” na vilima, “Tufunikeni!” ’ Kwa maana kama wamefanya hivi kwa mti mbichi, kwa mti mkavu itakuwaje?” Watu wengine wawili wahalifu, walipelekwa pamoja na Yesu ili wakasulubiwe. Walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, hapo ndipo walipomsulubisha Yesu pamoja na hao wahalifu, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui walitendalo!” Wakagawana nguo zake kwa kupiga kura. Watu wakasimama hapo wakimwangalia, nao viongozi wa Wayahudi wakamdhihaki wakisema, “Aliokoa wengine! Ajiokoe mwenyewe basi, kama yeye ndiye Kristo wa Mungu, Mteule wake.” Askari nao wakaja, wakamdhihaki. Wakamletea siki ili anywe, na wakamwambia, “Kama wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Kwenye msalaba juu ya kichwa chake, kulikuwa na maandishi haya: HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI. Maandishi haya yalikuwa yameandikwa kwa lugha za Kiyunani, Kilatini na Kiebrania.