Ayubu 27:1-12
Ayubu 27:1-12 SRUV
Kisha Ayubu akaendelea na hoja yake, na kusema, Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu; Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu; (Kwa kuwa uhai wangu ungali mzima ndani yangu, Na Roho ya Mungu iko katika pua yangu;) Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki, Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu. Hasha! Nisiwahesabie ninyi kuwa na haki; Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu. Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha; Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai. Adui yangu na awe kama huyo mwovu, Na mpinzani wangu awe kama asiye haki. Maana tumaini la mpotovu ni nini, ingawa ajipatia faida, Hapo Mungu amwondoleapo roho yake? Je! Mungu atakisikia kilio chake, Taabu zitakapomfikia? Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi, Na kumlingana Mungu nyakati zote? Nitawafundisha ninyi mambo ya mkono wa Mungu; Hayo yaliyo kwa Mwenyezi sitayaficha. Tazama, ninyi nyote mmeyaona wenyewe; Mbona basi mmebatilika kabisa?