Mwanzo 49:13-27
Mwanzo 49:13-27 SRUV
Zabuloni atakaa pwani ya bahari, Naye atakuwa kama pwani za kuegesha merikebu, Na mpaka wake utakuwa kando ya Sidoni. Isakari ni punda hodari, Ajilazaye kati ya mazizi ya kondoo; Akaona mahali pa raha, kuwa pema, Na nchi, ya kuwa ni nzuri, Akainama bega lake lichukue mizigo, Akawa mtumishi kwa kazi ngumu. Dani atahukumu watu wake, Kama moja ya makabila ya Israeli; Dani atakuwa nyoka barabarani, Bafe katika njia, Aumaye visigino vya farasi, Na apandaye akaanguka chali. Wokovu wako nimeungoja, Ee BWANA. Gadi, jeshi litamsonga, Lakini atawasonga wao mpaka visigino. Asheri, chakula chake kitakuwa kinono, Naye atatoa tunu za kifalme. Naftali ni ayala aliyefunguliwa; Anatoa maneno mazuri. Yusufu ni mti mchanga wenye kuzaa, Mti mchanga wenye kuzaa karibu na chemchemi, Matawi yake yametanda ukutani. Wapiga mishale walimtenda machungu, Wakamlenga na kumbana sana Lakini upinde wake ukakaa imara, Mikono yake ikapata nguvu, Kwa mikono ya Mwenye Enzi wa Yakobo; Kwa jina la mchungaji, yeye mwamba wa Israeli, Naam, kwa Mungu wa baba yako atakayekusaidia; Kwa baraka za juu mbinguni. Baraka za vilindi vilivyo chini, Baraka za maziwa, na za mimba. Baraka za baba yako Ni nyingi kuliko za milima ya kale, Vitu vinavyotamanika vya vilima vya milele; Na vikae juu ya kichwa cha Yusufu, Juu ya utosi wa kichwa chake, yeye aliyeteuliwa kati ya ndugu zake. Benyamini ni mbwamwitu mwenye kuraruararua Asubuhi atakula mawindo, Na jioni atagawanya mateka.